Kenya imeuchagua muungano unaojumuisha kampuni changa ya Marekani ya madini adimu (rare earths), ReElement Technologies, kuendeleza hifadhi ya madini muhimu ya Mlima Mrima, hatua inayoipa Washington rasilimali yenye thamani kubwa katika juhudi zake za kupata madini yanayotumika katika sekta ya ulinzi na vifaa vya kielektroniki.
Wizara ya Madini ya Kenya inasema tathmini za awali zinaonyesha kuwa Mlima Mrima, ulioko kusini-mashariki mwa nchi, una madini adimu yenye thamani ya makumi ya mabilioni ya dola, pamoja na niobium, metali inayotumika kutengeneza vyombo vya anga. Maafisa wa Marekani wameutaja mlima huo kuwa lengo muhimu katika mpango wa Rais Donald Trump wa kuongeza upatikanaji wa madini muhimu kwa Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara iliyotolewa Alhamisi, muungano wa Frontier Minerals unajumuisha kampuni za jimbo la Indiana, ReElement na American Resources Corporation, pamoja na kampuni ya uchimbaji madini ya Bunker Hill. Kabla ya kazi kuanza, muungano huo lazima ushirikiane na jamii za eneo hilo na kupata leseni za utafutaji madini. Huenda mradi ukakabiliwa na upinzani kwa kuwa eneo hilo liko ndani ya msitu unaochukuliwa kuwa mtakatifu na jamii za wenyeji.
Frontier imesema itajikita katika kujenga uwezo wa kuchakata na kusafisha madini nchini Kenya. “Tunakusudia kuunda fursa za kudumu kwa wafanyakazi wa Kenya, wafanyabiashara na uchumi kwa ujumla kupitia kujenga uwezo na uwekezaji unaolengwa, huku tukipa kipaumbele usimamizi na utendaji wa kimazingira,” alisema Brad Barnett, mwanachama msimamizi wa muungano huo.
Wazabuni saba waliorodheshwa mwezi Julai, lakini kampuni mbili za China zilijiondoa baadaye bila kutoa sababu. Katika duru ya mwisho, Frontier ilishindana na Mrima Earth Limited, inayojumuisha Critical Metals Corp na European Lithium, pamoja na kundi linaloongozwa na RareX ya Australia.
Jess Singh wa Mrima Earth Limited alisema muungano wake utapinga uamuzi huo mbele ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ya Kenya. RareX nayo ilisema itawasilisha pingamizi kabla ya Desemba 10, ikidai kuwa Frontier ilichelewa kuwasilisha barua ya nia ya kushiriki. Waziri wa Madini Hassan Ali Joho alisema atajibu madai ya RareX baadaye, huku wizara ikisisitiza kuwa mchakato ulikuwa huru na wa uwazi.
ReElement inapanga kutumia teknolojia mpya kusafisha madini adimu na madini mengine muhimu. Mwezi Julai, kampuni hiyo iliacha kuomba mkopo wa dola milioni 80 kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani baada ya kushindwa kukidhi masharti ya uchunguzi, lakini baadaye ilipewa ruzuku ya dola milioni 25 kutoka Pentagon ili kununua vifaa vya kiwanda chake cha Indiana.
Wakati huohuo, wizara ilitangaza kuwa ubia kati ya Fangda Special Steel Technology na Sinohydro Corporation umeshinda zabuni nyingine mbili za kuendeleza miradi ya chromite na shaba nchini Kenya.
Marekani imekuwa ikijaribu kupunguza ushawishi wa China katika sekta ya madini muhimu. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), China husafisha kati ya asilimia 47 na 87 ya shaba, lithiamu, kobalti, grafiti na madini adimu. Mwezi uliopita, Waziri Joho alisema Kenya haikupata “shinikizo lolote” kutoka Washington wala Beijing wakati wa mchakato wa zabuni ya Mlima Mrima.
Comments
0