Aliyekuwa msaidizi wa kiongozi wa upinzani wa Uganda aliyefungwa jela, Kizza Besigye, alifikishwa katika mahakama ya kijeshi jijini Kampala siku ya Jumatano akikabiliwa na shtaka la uhaini, zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuchukuliwa na watu wenye silaha.
Familia na wafuasi wa mwanaharakati huyo wa kisiasa, Sam Mugumya, wanasema hawakujua alipo tangu alipochukuliwa na watu wenye silaha kutoka hotelini mwezi Agosti 2025. Jeshi lilikuwa limekanusha hapo awali kuwa linamshikilia.
Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, aliandika kwenye mtandao wa X tarehe 2 Oktoba kwamba Mugumya yuko mikononi mwake, bila kueleza sababu.
Katika taarifa yake, jeshi lilisema Mugumya ameshtakiwa pamoja na wanajeshi wawili kwa makosa ya uhaini na mengine yanayohusiana na usalama. Watatu hao wanatuhumiwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya Uganda ambapo Mugumya “aliomba uungwaji mkono kutoka kwa wanajeshi ili kushirikiana na Allied Democratic Forces (ADF), kundi la waasi dhidi ya serikali ya Uganda.”
Kwa mujibu wa jeshi, Mugumya na washtakiwa wenzake wawili walikana mashtaka yote, na kila mmoja alipelekwa rumande katika magereza tofauti jijini Kampala.
ADF ni kundi la waasi wa Kiislamu lenye asili ya Uganda, ambalo lina makao yake katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kutoka huko, kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Uganda na dhidi ya malengo ndani ya Kongo.
Vyama vya upinzani pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakishinikiza Mugumya aachiliwe huru.
Comments
0