Klabu ya Italia, Como, ilionyesha kiwango cha kushangaza nchini Ufaransa baada ya kuichapa Lens mabao 9-0, na hivyo kufikia rekodi ya mabao mengi zaidi kufungwa na timu moja katika mechi moja ya Champions League. Ushindi huo unaongeza historia nyingine kwenye msimu wa kwanza wa kuvutia wa klabu hiyo barani Ulaya chini ya kocha Cesc Fàbregas.
Matokeo hayo yanalingana na ushindi wa Bayern Munich wa mabao 9-2 dhidi ya Dinamo Zagreb mwaka 2024. Hata hivyo, ushindi wa Como wa 9-0 ndio mkubwa zaidi kuwahi kupatikana ugenini katika historia ya Champions League.
Como pia imekuwa timu ya tatu tu tangu mashindano hayo yaanze kushinda kwa tofauti ya mabao manane, ikiungana na Liverpool na Real Madrid, ambazo zilipata ushindi wa 8-0 nyumbani dhidi ya Besiktas na Malmo mtawalia. Aidha, ni timu ya kwanza kufunga mabao tisa ugenini katika mechi ya Kombe la Ulaya tangu Feyenoord ilipoichapa Olympiakos Nicosia 9-0 mwezi Septemba 1971.
Licha ya mafanikio hayo, Feyenoord bado inashikilia rekodi ya jumla ya mabao katika Kombe la Ulaya baada ya kuifunga timu ya Iceland, KR, mabao 12-2 mwezi Septemba 1969.
Rekodi ya ufungaji ya Como imekuwa ya kipekee vilevile. Hakuna timu iliyowahi kufunga zaidi ya mabao 19 ambayo Como imefunga katika mechi zake nne za kwanza za mashindano ya Ulaya; ni Queen’s Park Rangers pekee waliofikia kiwango hicho katika kampeni ya Kombe la UEFA msimu wa 1976-77.
Ushindi dhidi ya Lens umeipandisha Como hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa hatua ya ligi ya Champions League, baada ya ushindi wa awali dhidi ya RB Leipzig na Manchester United, huku kipigo chembamba kutoka kwa Feyenoord kikiwa doa pekee katika mwenendo wao mzuri.
Aliyekuwa beki wa Manchester City, Nedum Onuoha, aliyasifu maendeleo ya klabu hiyo, akiyaita mafanikio yake ya ajabu ukizingatia uzoefu wake mdogo barani Ulaya.
“Wanachokifanya kinavutia sana, ukizingatia kuwa hii ni mara yao ya kwanza barani Ulaya,” Onuoha aliiambia BBC Sport.
“Kwa kweli, nakumbuka walipopanda daraja kwa mara ya kwanza na kulikuwa na habari nyingi mitandaoni za Fàbregas akifurahia sana, na walikuwa wakipigania maisha yao katika vita vikali vya kukwepa kushuka daraja.
“Misimu miwili baadaye na pengine, pamoja na PSG na Barcelona, wao ni timu tatu zinazosisimua zaidi katika Champions League.”
Kupanda kwa klabu hiyo kunashangaza zaidi ukizingatia kuwa hivi karibuni tu, katika msimu wa 2018-19, ilikuwa ikicheza Serie D, daraja la nne la soka la Italia.
Mabadiliko yake yalifuatia ununuzi wa klabu hiyo uliofanywa na kampuni ya habari yenye makao yake London, Sent Entertainment, inayomilikiwa na mabilionea wa Indonesia, ndugu Robert Budi Hartono na Michael Bambang Hartono.
Mkataba huo ulipokamilika mwaka 2019, ndugu hao awali walipanga mradi wa televisheni ambao ungeonyesha mechi zinazowahusisha wachezaji chipukizi wa Indonesia kwa watazamaji wa nyumbani. Hata hivyo, kupanda daraja kwa klabu bila kutarajiwa kulibadilisha mipango hiyo.
“Kwa namna fulani timu ilipanda daraja, tukalazimika kuwa wa kulipwa (professional), na mpango ukalazimika kufutwa,” mtendaji mkuu Mirwan Suwarso aliiambia Piers Morgan’s Football Uncensored Podcast mwezi Oktoba.
Licha ya uungwaji mkono wa kifedha, kasi ya maendeleo ya Como imewashangaza wachambuzi, huku aliyekuwa beki wa Liverpool, Stephen Warnock, akisisitiza kuwa uwekezaji peke yake hauhakikishi mafanikio.
“Ndiyo, wana wamiliki matajiri lakini hilo pekee halikununulii mafanikio ya uhakika,” Warnock aliiambia BBC Sport.
“Lazima ununue wachezaji sahihi wanaoendana na mfumo sahihi, na Fàbregas amechagua pia wachezaji vijana, ambao wana njaa ya mafanikio lakini pia wanaweza kuendelea kupiga hatua na kuendelea kuimarika, kama yeye alivyo kama kocha.
“Kwa hiyo maendeleo ya timu karibu yanaakisi maendeleo yake, kwa namna ambavyo watapiga hatua pamoja. Ni hadithi nzuri sana.”
Comments
0