Ethiopia na Sudan zimefunga ofisi za ubalozi mdogo (consulates) za kila mmoja zilizoko karibu na mpaka wao wa pamoja, maafisa wa nchi hizo mbili walisema Jumatano. Hatua hiyo inaashiria kuzorota zaidi kwa uhusiano kati ya majirani hao, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kuwasaidia maadui zake.
Sudan inaituhumu Ethiopia kuunga mkono kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), huku Ethiopia nayo ikiishutumu Sudan kwa kuwaunga mkono waasi katika eneo lake la kaskazini la Tigray. Pande zote mbili zinakanusha tuhuma hizo, lakini mvutano huu umezua hofu kwamba vita hivyo viwili vinaweza kuingiliana na kuzaa mzozo mpana zaidi katika Pembe ya Afrika.
Addis Ababa inakanusha kuisaidia RSF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, mzozo huo umewalazimu zaidi ya watu milioni 14 kuyakimbia makazi yao na umesababisha mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani tangu ulipozuka Aprili 2023.
Ethiopia, kwa upande wake, imezituhumu Sudan, Misri na Eritrea kuwaunga mkono waasi wa Tigray, ambao walianzisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali mwezi Septemba. Nchi zote tatu zimekanusha madai hayo.
Jumapili, serikali ya Sudan ilitangaza kuwa imewasilisha malalamiko dhidi ya Ethiopia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika. Sudan inaishutumu Ethiopia kwa kuiruhusu RSF kutumia ardhi yake kurusha droni za kujitoa mhanga (suicide drones) dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini Sudan.
Msemaji wa ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia hakujibu ombi la Reuters la kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Ethiopia aliyezungumza na Reuters, Ethiopia ilifunga ubalozi mdogo wa Sudan katika mji wa mpakani wa Assosa na kuwaamuru wanadiplomasia sita waliokuwa wakifanya kazi hapo kuondoka ndani ya saa 48. Afisa huyo hakueleza sababu ya uamuzi huo.
Baadaye, serikali ya Sudan ilijibu kwa kufunga ubalozi mdogo wa Ethiopia katika mji wa Gedaref, mashariki mwa Sudan, na kuwafukuza wanadiplomasia waliokuwa wakihudumu hapo, maafisa wawili wa Sudan waliiambia Reuters. Maafisa hao waliomba majina yao yasitajwe kwa kuwa walikuwa wakizungumzia suala nyeti la kidiplomasia.
Amjad Farid, mshauri wa masuala ya kisiasa na mambo ya nje wa Baraza la Mpito la Mamlaka ya Sudan (Transitional Sovereignty Council), alieleza msimamo wa serikali yake: “Serikali ya Sudan inaendelea kushikilia haki yake ya kulinda ardhi yake. Hata hivyo, inafanya kila juhudi inayowezekana kuepuka vita vya wazi na Ethiopia.”
Comments
0