Chama kikuu cha upinzani nchini India, Congress, kimefanya maandamano nje ya ofisi za Meta katika miji kadhaa, kufuatia kuondolewa kwa akaunti za Instagram za baadhi ya wanachama wake. Kwa mujibu wa video zilizotolewa Jumamosi na tawi la vijana la chama hicho, Indian Youth Congress, wanachama wake walikabiliana na polisi na walinzi wakati wa maandamano katika miji ya Hyderabad, Mumbai na Gurugram.
Maandamano hayo yamezidisha mvutano kati ya kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii na chama hicho cha upinzani, kufuatia madai ya udhibiti wa kisiasa na vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza mtandaoni. Meta ilikataa kuzungumzia maandamano hayo, ambayo yanaashiria kupanuka kwa mzozo wake na Congress nchini India, soko lake kubwa zaidi kwa idadi ya watumiaji.
Congress imekuwa ikizituhumu mara kwa mara Meta na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii kwa kukandamiza sauti za upinzani kwa kuzuia akaunti na maudhui yanayoikosoa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi. Hata hivyo, serikali inashikilia kuwa amri za kuondoa maudhui hutolewa pale tu maudhui hayo yanapokiuka sheria za India au kutishia usalama wa umma na usalama wa taifa. Meta nayo imesema vikwazo vyake vinalenga kuhakikisha inatii kanuni za ndani.
Huko Hyderabad siku ya Ijumaa, waandamanaji waliobeba mabango waliingia katika eneo la jengo lenye ofisi za Meta, wakiimba kauli mbiu na kukabiliana na polisi. Video iliyosambazwa na Indian Youth Congress ilimwonyesha mwandamanaji mmoja akivunja chungu cha maua huku walinzi wakijaribu kudhibiti hali.
Mjini Mumbai, video nyingine ilionyesha wafuasi wa Congress wakipuliza rangi na kuandika jumbe za kuipinga Meta kwenye kuta za jengo lenye ofisi za kampuni hiyo. Waandamanaji hao pia walikabiliana na walinzi waliojaribu kuwazuia.
Huko Gurugram, karibu na New Delhi, wanachama wa chama hicho walifanya maandamano mengine wakiwa na mabango yanayodai akaunti zilizozuiwa zirejeshwe.
Awali, Indian Youth Congress ilikuwa imetishia kuandaa maandamano katika ofisi za Meta kote nchini iwapo akaunti za viongozi wake hazingerejeshwa.
Akizungumza na Reuters Jumamosi, Manu Jain, anayesimamia shughuli za mitandao ya kijamii za tawi hilo la vijana, alisema akaunti mbili zilirejeshwa baada ya maandamano ya Ijumaa. Hata hivyo, alidai kuwa maelfu ya akaunti za waandishi wa habari, watengenezaji maudhui na washawishi (influencers) wanaoikosoa serikali bado zimezuiwa.
Jain aliitaka Meta ieleze jinsi algorithimu (algorithms) zake zinavyoamua maudhui yapi yazuiwe, na akadai kurejeshwa kwa akaunti zilizoondolewa kufuatia maagizo ya serikali.
Maandamano haya yanakuja wakati kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu udhibiti wa mtandaoni na uhuru wa kujieleza nchini India. Watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari wanaonya kuwa vikwazo vya serikali vinazidi kupunguza uwezo wa majukwaa ya mitandao ya kijamii kuchunguza maombi ya kuondoa maudhui.
Shirika la Reporters Without Borders limeripoti ongezeko la kuondolewa kwa maudhui ya kihabari kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii nchini India mwaka huu.
Mwezi Februari, serikali ya India ilianzisha masharti makali zaidi yanayozitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuondoa maudhui yaliyo kinyume cha sheria ndani ya saa tatu baada ya kupokea maagizo halali ya serikali au mahakama, badala ya muda wa awali wa saa 36.
Kanuni hizo mpya zimeibua wasiwasi miongoni mwa kampuni za teknolojia kuhusu muda mfupi uliopo wa kupitia na kuthibitisha maombi ya kuondoa maudhui.
Takwimu zilizotolewa na Meta zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilizuia zaidi ya machapisho au akaunti milioni 5.4 nchini India chini ya sheria za ndani katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026. Idadi hiyo ilikuwa ya pili kwa ukubwa duniani, nyuma ya Indonesia, na ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na takriban vizuizi 70,000 vilivyorekodiwa katika miezi sita iliyotangulia.
Meta ilisema vizuizi vingi vilihusu maudhui ambayo ilitakiwa kisheria kuyaondoa chini ya kanuni za ndani za India.
Comments
0