Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Msumbiji, Venancio Mondlane, alianza kusikilizwa kesi yake siku ya Jumanne, akikabiliwa na mashtaka ya kuchochea ugaidi na uasi wa kiraia kufuatia vurugu zilizosababisha vifo baada ya uchaguzi tata wa mwaka 2024.
Mondlane amekanusha mashtaka yote yanayomkabili, akisema kesi dhidi yake imechochewa na siasa. Akizungumza na waandishi wa habari, alisema anajihisi mtulivu na mwenye kujiamini kutokana na kazi iliyofanywa na mawakili wake.
Kwa mujibu wa kundi moja la asasi za kiraia linalofuatilia hali hiyo, zaidi ya watu 300 waliuawa katika maandamano ya baada ya uchaguzi. Hayo yalikuwa maandamano makubwa zaidi kuwahi kufanyika dhidi ya Frelimo, chama tawala kilichoshika madaraka tangu uhuru mwaka 1975.
Upinzani unadai kuwa Rais Daniel Chapo na Frelimo walishinda uchaguzi huo kwa kuiba kura, tuhuma ambazo rais na chama tawala wanazikataa. Wakati huo, waangalizi wa nchi za Magharibi walisema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Siku ya Jumanne, maafisa wa polisi na magari yao walisambazwa katika barabara zote zinazoelekea Mahakama Kuu, ambako kesi hiyo ilianza. Kesi hiyo inatarajiwa kuchukua miezi kadhaa. Makumi ya wafuasi wa Mondlane walikusanyika nje ya mahakama, wakiliita jina lake na kumpungia mikono alipojitokeza.
Mahakama imepiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya kesi hiyo, ikitaja hatari ya kuzuka kwa machafuko. Saa mbili za kwanza za kesi zilitumika kushughulikia masuala ya kiutaratibu, wakati mawakili wa Mondlane walipojaribu kuyafuta mashtaka dhidi yake, lakini mahakama ilikataa hoja zao.
Comments
0