Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya, Benni McCarthy, amewajibu kwa nguvu wale wanaohoji kazi yake, akisisitiza kuwa ukosoaji huo haumsumbui hata kidogo na kwamba ameridhika na mafanikio yake binafsi na ya kitaaluma.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu lawama kutoka kwa baadhi ya Wakenya, akiwalenga hasa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhoji uwezo wake wa ukocha na maamuzi anayofanya.
“Ninaporudi nyumbani, naweka kichwa changu kwenye mto, nalala kama mtoto. Maisha yangu yamekamilika. Sihitaji kuhangaika kuhusu maji ya moto, lakini mtu aliyekaa na simu yake, labda hajala kwa wiki mbili, anaweza haraka kusema, ‘Aah, yule kocha…’” alisema McCarthy.
Kauli za mtaalamu huyo wa mbinu kutoka Afrika Kusini zinaonyesha wazi uchovu wake kutokana na kuchunguzwa kila mara, hasa na watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao, kwa mtazamo wake, ukosoaji wao hauakisi uelewa wa mahitaji halisi ya soka la kulipwa.
Kabla ya kukabidhiwa timu ya taifa ya Kenya, McCarthy alihudumu kama kocha wa washambuliaji wa kikosi cha kwanza cha Manchester United. Alichukua mikoba ya Harambee Stars akiwa na jukumu la kuboresha matokeo ya soka la nchi hiyo.
Kauli zake hizi mpya zinatarajiwa kuzua mjadala zaidi miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Kenya, hasa wale ambao wamekuwa wakihoji matokeo na mtindo wake wa uongozi tangu aanze kuinoa Harambee Stars.
Comments
0