Mamlaka za mashariki mwa Libya zimetangaza kukamata zaidi ya vidonge milioni 4 vya kulevya pamoja na kilo 29 za kokeini na bangi aina ya hashish katika mji wa pwani wa Derna siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Idara Kuu ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Wizara ya Mambo ya Ndani, wanachama wa genge linalojihusisha na biashara ya dawa za kulevya walikamatwa mjini humo.
Picha zilizochapishwa na idara hiyo zilionyesha marundo ya vipande vya hashish, maboksi na mifuko ya plastiki inayoonekana ndani yenye vidonge vyeupe.
Katika taarifa ya video iliyochapishwa usiku wa Jumanne, mkurugenzi wa idara hiyo, Meja Jenerali Ahmed Al-Shamikh, alitoa onyo kali. “Hatutaonyesha huruma yoyote kwa mtu yeyote atakayethubutu kuhatarisha usalama wa vijana wetu au mustakabali wa nchi yetu,” alisema.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Januari inaeleza kuwa Libya imekuwa kitovu kikubwa cha kikanda cha kupitishia dawa za kulevya za kemikali (synthetic drugs) na aina nyingine, zinazowafikia watumiaji wa ndani na kusambazwa katika maeneo mengine ya Afrika Kaskazini na bara zima. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inasema magenge ya dawa za kulevya yamekuwa yakitumia fursa ya hali ya machafuko nchini humo tangu mwaka 2011.
Mwaka 2011, Gaddafi aliangushwa katika uasi ulioungwa mkono na NATO, hatua iliyoitumbukiza Libya katika kipindi kirefu cha mizozo ya ndani na mgawanyiko. Miaka mitatu baadaye, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka kati ya makundi yenye silaha yaliyokuwa yakiwania madaraka, na nchi ikagawanyika kati ya tawala za mashariki na magharibi.
Comments
0