Mtayarishaji wa maudhui kutoka Kenya, Bradley Marongo, anayefahamika zaidi kama Gen Z Goliath, amepaza sauti baada ya Meta kushikilia kwa miezi mitatu mapato yake ya Facebook yanayozidi KSh 300,000 (takriban dola 2,536 za Marekani, kwa kiwango rasmi cha Benki Kuu ya Kenya cha KSh 129.99 kwa dola moja). “Meta, kwa nini mnakataa kunilipa pesa zangu nilizozitolea jasho?” aliuliza.
Marongo anasema Meta ilisitisha malipo kwenye ukurasa wake baada ya mfumo wake kudai kuwa ulibaini mwingiliano usio halisi, wakati alipokuwa Afrika Kusini akitengeneza vichekesho pamoja na William Last KRM. Ukurasa huo ulinyimwa malipo na kupunguziwa usambazaji wa maudhui kwa miezi mitatu, adhabu iliyomalizika tarehe 24 Oktoba 2026. “Inawezekanaje ushiriki halisi wa hadhira ghafla uitwe si halisi?” alihoji.
Kwa mujibu wa takwimu za dashibodi yake, takriban dola 1,900 zilikusanywa kabla ya adhabu, na dola 636 nyingine zilipatikana baada ya ukurasa kurejeshwa. Wiki tatu baada ya kurejeshwa, hali ya malipo ilibadilika ghafla: “Hali ya malipo ilibadilika kutoka ON HOLD hadi NOT PAYABLE.” Marongo anashangaa kwa nini hata pesa alizopata baada ya kurejeshwa nazo zimezuiliwa.
Anasema aliwasiliana mara kwa mara na timu ya msaada ya Meta kwa miezi mitatu bila mafanikio. “Jibu kutoka kwa timu ya msaada ni kwamba suala hili liko nje ya uwezo wao na kwamba wao si wanaohusika kufanya uamuzi wa mwisho.”
Marongo ameiomba Wizara ya TEHAMA, sekta ya uchumi wa kidijitali na taasisi za kitaifa za kulinda watumiaji kuchunguza changamoto zinazowakabili watayarishaji wa maudhui kwenye majukwaa ya kimataifa. “Tunahitaji uwazi, uwajibikaji na njia sahihi kwa watayarishaji wa maudhui kukata rufaa dhidi ya maamuzi yanayoathiri riziki zao.”
Amesisitiza kuwa kutengeneza maudhui kunahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa, usafiri, intaneti, uhariri na timu za uzalishaji. “Tunaenda wapi sisi kama watayarishaji wa maudhui wa Kiafrika?” aliuliza. Hadi sasa, Meta haijatoa taarifa yoyote kwa umma kuhusu malipo yake.
Comments
0