Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), Volker Türk, ameonya kuwa ubaguzi wa rangi bado unaathiri upatikanaji wa ajira, huduma za afya, makazi na haki kwa Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika, na ametoa wito wa haki ya fidia (reparatory justice) ili kukabili athari za kudumu za utumwa na ukoloni.
Akihutubia mjadala wa ngazi ya juu kuhusu haki ya fidia mjini Geneva siku ya Alhamisi, Türk alisema taasisi, ukosefu wa usawa wa kiuchumi na teknolojia mpya kama akili bandia (AI) zinaimarisha ubaguzi wa kimfumo. “Akili bandia na teknolojia nyingine, na tumekuwa tukilizungumzia hili kwa sauti kubwa, tayari zinazalisha upya upendeleo wa binadamu. Tusipokuwa makini, zinaweza kuzidisha ubaguzi wa kimfumo dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika,” alisema.
Alieleza kuwa katika maeneo mbalimbali, polisi wana uwezekano mara kadhaa zaidi wa kutumia nguvu dhidi ya watu wenye asili ya Kiafrika, ambao pia ni wengi kupita kiasi magerezani katika nchi nyingi. “Muundo wa kidemografia wa magereza ni ishara ya ni nani tunaowatenga,” alisema.
Türk alihusisha unyonyaji wa kihistoria na ukosefu wa usawa wa kiuchumi duniani leo, akibainisha kuwa nchi nyingi zinazoendelea, zikiwemo zilizokuwa makoloni, zinakabiliwa na madeni yasiyohimilika. Alitaka mageuzi katika mfumo wa fedha wa kimataifa ili kupunguza mzigo wa madeni na kuzipa nchi za Afrika sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya uchumi wa dunia.
“Haki ya fidia ina sura nyingi na haipaswi kuchanganywa na fidia ya kifedha pekee,” alisema Türk. Alitaja hatua kama kuomba radhi rasmi, juhudi za kutafuta ukweli, kumbukumbu, kurejesha vitu vya kitamaduni, elimu na msaada wa kiafya na kisaikolojia, huku akionya kuwa hakuna nchi iliyokwisha kuwajibika kikamilifu kwa madhara ya kihistoria. Aliongeza kuwa chini ya robo ya nchi ndizo zenye sheria kamili za kupinga ubaguzi.
Alisisitiza kuwa Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika, hasa wanawake, lazima wawe kitovu cha maamuzi kuhusu haki ya fidia. “Mtoto aliyezaliwa mwaka 2026 hapaswi kubeba mzigo wa karne nyingi za ubaguzi wa rangi na maovu ya zamani,” alisema Türk.
Comments
0