Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh aliyeng’olewa madarakani, Sheikh Hasina, ametangaza mpango wa kurejea nyumbani Desemba 16 baada ya kuishi uhamishoni nchini India kwa zaidi ya miaka miwili. Tarehe hiyo ni kumbukumbu ya kumalizika kwa vita vya ukombozi vya Bangladesh vya mwaka 1971, kwa mujibu wa msemaji wake aliyezungumza Jumanne.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79 kutaja tarehe mahususi ya kurejea, hatua inayoweza kuzidisha mvutano wa kisiasa na kisheria katika nchi ambayo chama chake bado kimepigwa marufuku. Mvutano ulianza mapema mwezi huu alipoomba pasipoti mpya na nyaraka zinazohusiana, ambazo zilifutwa baada ya kukimbilia Delhi kufuatia uasi uliomwondoa madarakani.
Msemaji wake, Syed Mozammel Ali, alisema Hasina sasa anaitaka serikali ya Bangladesh impangie safari ya kurudi nyumbani kwa ndege ya shirika la taifa, Biman Bangladesh Airlines, akikumbusha kuwa alisafirishwa kwenda India kwa ndege ya Bangladesh Agosti 5, 2024.
“Baada ya kumpeleka uhamishoni kinyume na Katiba katika mazingira kama hayo, sasa ni wajibu wa serikali kuwezesha kurejea kwake Bangladesh katika Siku ya Ushindi, Desemba 16,” alisema.
Serikali ya Bangladesh ilikataa ombi hilo moja kwa moja, ikisisitiza kuwa Hasina anaweza kurudi tu kupitia mchakato wa kurejeshwa kutoka India (extradition). Mwaka jana, mahakama ya Bangladesh ilimhukumu kifo bila yeye kuwepo, kutokana na ukandamizaji mbaya dhidi ya uasi ulioongozwa na wanafunzi, mashtaka ambayo ameyakanusha akiwa uhamishoni.
“Hasina ni mhalifu aliyetiwa hatiani; gaidi aliyetoroka,” alisema Humaiun Kobir, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Bangladesh. “Anaweza kurudi nyumbani tu kwa mkataba wa kurejesha wahalifu; akiwa amefungwa pingu, na chini ya ulinzi mkali.” Kuhusu ombi la ndege, aliongeza: “Bangladesh haitashughulikia ombi lolote la kufikirika kama hilo.”
Aminul Islam, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Bangladesh, iliyotoa hukumu ya kifo dhidi ya Hasina, alisema si busara kwa mtoro aliyetiwa hatiani kutarajia serikali impangie safari ya kurudi. Waziri mmoja wa Bangladesh alisema Jumapili kuwa Hasina atakamatwa na kufungwa jela mara tu atakapowasili, akiongeza kuwa hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika na India kuhusu kutuma ndege kumchukua.
Wizara ya Mambo ya Nje ya India haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni. Mwezi Aprili, ilisema inapitia ombi la Bangladesh la kumrejesha Hasina, na kwamba inataka “kushirikiana kwa njia ya kujenga na serikali mpya na kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.”
Umoja wa Mataifa umesema hadi watu 1,400 waliuawa wakati wa machafuko yaliyomlazimisha Hasina kuondoka madarakani.
Comments
0