Madai ya vifo vya wachimbaji wadogo wawili waliokuwa wakichimba kinyume cha sheria, wanaotambulishwa tu kama ZZZ na ZZY, waliopigwa risasi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara nchini Tanzania, ndiyo kiini cha kesi dhidi ya Chama cha Soko la Dhahabu cha London (London Bullion Market Association – LBMA) iliyoanza jijini London siku ya Jumatano, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama za pande zote mbili.
Kesi hiyo ya wiki sita inalenga kubaini iwapo LBMA, ambayo ni taasisi ya sekta ya dhahabu, inaweza kuwajibishwa kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na mnyororo wa usambazaji wa dhahabu. LBMA inakanusha madai hayo.
Walalamikaji, wanaojulikana kama AAA na AAB, wanakiri kuwa LBMA haikuwa na mamlaka juu ya polisi wa Tanzania, lakini wanasema hilo haliiondolei jukumu la kuchukua tahadhari (duty of care) kuhusu mnyororo huo wa usambazaji.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, walalamikaji wanasema vijana hao wawili walikuwa wachimbaji wadogo na wakulima waliojiajiri, ambao waliongeza kipato chao kupitia uchimbaji usio na leseni na usio halali.
Walalamikaji wanadai kuwa wote wawili walipigwa risasi na polisi walipokuwa wakikimbia kutoka mgodini katika matukio tofauti mwaka 2019, na kwamba hakuna hata mmoja aliyekuwa tishio.
Kuhusu ZZZ, walalamikaji wanasema alikuwa ameacha panga lake nyumbani na hakuwa na silaha yoyote wakati polisi walipofyatua risasi. Kuhusu ZZY, ndugu na mashahidi wanadai kuwa alipigwa risasi mgongoni alipokuwa akikimbia, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama.
Walalamikaji wanadai kuwa vifo hivyo vilikuwa sehemu ya mwenendo mpana wa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wakazi wa eneo hilo wanaoingia mgodini kutafuta mabaki yenye dhahabu.
Pia wanapinga utetezi unaotegemea uharamu wa kitendo cha kuingia mgodini, wakisema kuwa wanaoingia bila ruhusa hawapotezi ulinzi wa sheria ya kawaida (common law), na kwamba matumizi yoyote ya nguvu lazima yabaki ndani ya mipaka ya busara.
Kwa upande wake, LBMA inaangazia historia ndefu ya mgodi wa North Mara ya kuvamiwa na makundi makubwa ya wachimbaji haramu, wakati mwingine yakihusisha mamia au hata maelfu ya watu. Nyaraka za mahakama zinaeleza kuwa wavamizi hao mara kadhaa wamekuwa wakibeba mapanga.
Aidha, LBMA inaonyesha kile inachokiita mapengo katika ushahidi. Katika nyaraka zake za mahakama, inasema walalamikaji hawajaomba kumbukumbu za matukio wala ripoti kutoka kwa polisi wa Tanzania, wakitaja hofu ya kulipizwa kisasi, na hawajawasilisha ushahidi wa kitabibu wala ripoti za uchunguzi wa maiti kuthibitisha madai muhimu kuhusu vifo hivyo.
Wawakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania hawakujibu maombi ya kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Comments
0