Vyanzo viwili vinavyofahamu moja kwa moja kuhusu uhamisho huo vinasema Hezbollah ilipokea dola milioni 200 kutoka Iran mwezi uliopita ili kuwasaidia raia wa Lebanon waliolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita na Israel.
Marekani imepinga madai hayo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tommy Pigott, alisema fedha hizo “hazipo” na akaishutumu Hezbollah kwa kujaribu “kujisafisha kwa hadithi za uongo kuhusu mamilioni ya fedha kutoka Iran.” Wizara ya Fedha ya Marekani nayo ilisema Iran inaishiwa fedha na njia za kuzihamisha.
“Marekani itaendelea kuzibana fedha za Hezbollah kupitia vikwazo huku ikiunga mkono uwezo wa serikali halali ya Lebanon kujenga upya eneo la Kusini,” alisema Pigott.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Hezbollah inapanga kutoa malipo ya awali ya dola 3,000 kwa kila familia iliyoathirika, kwa kuzipa kipaumbele familia ambazo vijiji vyao vimeharibiwa au haviwezi kufikiwa kutokana na uvamizi wa Israel. Takriban familia 50,000 zinatarajiwa kunufaika. Afisa mmoja wa Hezbollah alithibitisha kupatikana kwa fedha hizo bila kutaja chanzo chake.
Vyanzo vilisema wapatanishi walitoza ada ya asilimia 20 kuhamisha fedha hizo, mara nne ya kiwango cha kawaida, kutokana na hatari iliyopo. Kampuni za Iraq na Dubai zilizokuwa zikifanya uhamisho huo hazipatikani tena, na zile za Uturuki nazo zinakabiliwa na shinikizo. Wizara ya Fedha ya Marekani inasema Iran iliihamishia Hezbollah dola bilioni 1 katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka 2025, ingawa Tehran haijawahi kukiri kuifadhili.
Mashambulizi ya Israel yamewafanya mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao tangu Hezbollah ilipojiunga na vita vya kikanda kuiunga mkono Iran Machi 2. Wizara ya afya ya Lebanon inasema zaidi ya watu 4,300 wameuawa tangu wakati huo, huku Waziri Mkuu Nawaf Salam akikadiria kuwa ujenzi mpya kufuatia vita viwili tangu mwaka 2024 unaweza kugharimu zaidi ya dola bilioni 27.
Comments
0