Mashambulizi mawili yaliyotokea magharibi mwa Niger, nchi isiyo na bahari katika ukanda wa Sahel, yamesababisha vifo vya zaidi ya askari 50 wa vikosi vya usalama, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya usalama. Eneo hilo lina harakati za makundi ya wanajihadi, wakiwemo wafuasi wa tawi la kikanda la Islamic State.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, msafara wa askari wa jeshi la polisi (gendarmes) ulishambuliwa kwa kuviziwa karibu na mji wa Abala-Filingué Jumatano ya wiki iliyopita. Siku ya Jumamosi, shambulizi jingine katika mji wa Birni-N'Konni liliua zaidi ya wanajeshi 30.
Vyanzo hivyo vilieleza kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa na magaidi, bila kutoa maelezo zaidi.
Tawi la Islamic State katika Afrika Magharibi, linalojulikana kama Islamic State Sahel Province, lilitoa taarifa mbili Jumapili likidai kuhusika na mashambulizi hayo, kwa mujibu wa SITE Intelligence Group iliyoripoti Jumatatu.
Mwezi Januari, kundi hilo lilishambulia uwanja wa ndege wa kiraia na kambi ya jeshi la anga mjini Niamey, mji mkuu wa nchi hiyo. Tukio hilo lilidhihirisha jinsi serikali inayoongozwa na jeshi, iliyonyakua madaraka kwa mapinduzi mwaka 2023, isivyopiga hatua katika mapambano dhidi ya makundi ya waasi.
Mwezi uliopita, wanajeshi waasi nchini Niger walishambulia uwanja wa ndege na ikulu ya rais, hali iliyozua mvutano na vikosi vitiifu kwa serikali. Vikosi hivyo vilisaidiwa na wanajeshi wa Africa Corps, kikosi cha kijeshi kinachodhibitiwa na Kremlin.
Wachambuzi na vyanzo vya usalama wanasema hasira inazidi kuongezeka miongoni mwa vitengo vya jeshi vilivyo mstari wa mbele baada ya kupata hasara za mara kwa mara mikononi mwa waasi, hasa magharibi mwa Niger.
Comments
0