Watu wasiopungua 11 wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya watu watatu wenye silaha kuvamia sherehe iliyokuwa ikifanyika nyumbani na kuanza kufyatua risasi nchini Afrika Kusini.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumanne katika kitongoji cha KwaMakhutha, takriban kilomita 30 kusini mwa jiji la Durban, jimboni KwaZulu-Natal. Kwa mujibu wa polisi, waathiriwa walikuwa wamekusanyika katika nyumba hiyo kwa ajili ya sherehe wakati washukiwa walipoingia na kuwamiminia risasi.
Watu kumi, akiwemo mwanamke anayeaminika kuwa mjamzito, walifariki papo hapo, huku mwathiriwa wa kumi na moja akifariki baadaye akiwa hospitalini.
Hali ya majeruhi hao watatu haikufahamika mara moja. Polisi walisema wanaendelea kuwasaka washambuliaji, na kwamba hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi sasa.
Sababu ya shambulio hilo bado haijathibitishwa. Polisi walieleza kuwa baadhi ya watu waliokuwa katika nyumba hiyo walikuwa wanafahamika kwa vyombo vya usalama kutokana na uchunguzi wa makosa ya jinai, ingawa walikataa kutoa maelezo zaidi.
“Ingawa sababu ya ufyatuaji risasi huo bado haiwezi kuthibitishwa, uhasama kati ya makundi hasimu hauwezi kuondolewa katika uwezekano,” polisi walisema.
Mamlaka pia zinachunguza iwapo gari lililochomwa moto karibu na nyumba hiyo lina uhusiano wowote na shambulio hilo.
Waziri Mkuu wa jimbo la KwaZulu-Natal, Thami Ntuli, aliyaelezea mauaji hayo kuwa “yanasikitisha sana” na akasema jamii hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo yanayojulikana ya biashara ya dawa za kulevya na silaha haramu.
Shambulio hili ni la hivi karibuni katika mfululizo wa mauaji ya halaiki yanayoikumba Afrika Kusini. Mwezi Juni, watu kadhaa wenye silaha waliwaua watu 12 katika mtaa maskini jijini Johannesburg, huku mashambulio mawili ya risasi yaliyotokea kwa tofauti ya wiki mbili mwezi Desemba yakiacha watu 21 wakiwa wamekufa.
Takwimu rasmi za polisi zinaonyesha kuwa mauaji 5,427 yalirekodiwa kati ya Aprili na Juni — wastani wa karibu mauaji 60 kwa siku. Ufyatuaji risasi ndio njia inayotumika zaidi katika mauaji nchini humo, na polisi pamoja na wataalamu wa uhalifu wanataja kusambaa kwa wingi kwa silaha haramu kuwa chanzo kikuu cha viwango vya juu vya uhalifu wa kutumia nguvu.
Katika eneo la tukio huko KwaMakhutha, miili ya baadhi ya waathiriwa iliwekwa nje ya nyumba na kufunikwa kwa shuka nyeupe wakati wachunguzi wa kitaalamu wa uhalifu (forensic) wakikagua eneo hilo. Polisi walizingira mtaa mzima unaozunguka nyumba hiyo wakati uchunguzi ukiendelea.
Comments
0