Watu wasiopungua wanne wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa vibaya kwa moto baada ya mlipuko kutokea Jumatatu asubuhi katika kiwanda cha kuyeyusha chuma jijini Douala, mji mkuu wa kibiashara wa Cameroon, kwa mujibu wa gavana wa mkoa.
Samuel Dieudonne Ivaha Diboua, gavana wa Mkoa wa Littoral ambao makao yake makuu ni Douala, alisema mlipuko huo ulisababisha moto ambao baadaye ulizimwa.
Metafrique Steel, kampuni ya utengenezaji na biashara yenye makao yake Douala, ilithibitisha kuwa vituo vyake vilivyoko katika Eneo la Viwanda la Bassa (Bassa Industrial Park) viliathirika. Kampuni hiyo ilieleza kuwa kulitokea “tukio, lililosababishwa na sababu ya nje na ambalo chanzo chake bado hakijabainika,” bila kutoa maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa Diboua, kikosi cha uokoaji cha jeshi ndicho kilichoopoa miili ya watu wanne waliopoteza maisha, kama alivyowaeleza waandishi wa habari.
“Katika eneo la kiwanda, majeruhi 16 walioungua waliokolewa na kupelekwa katika Hospitali Kuu ya Douala (Douala General Hospital) ...,” alisema gavana huyo.
Gavana huyo alionya kuwa hali ya waliojeruhiwa bado ni tete: “Hatupaswi kuwa na matumaini makubwa kupita kiasi kutokana na ukubwa wa majeraha ya moto,” Diboua aliongeza.
Comments
0