Wabunge nchini Senegal siku ya Ijumaa walikataa kwa mara ya pili bajeti iliyorekebishwa, ambayo ni muhimu ili nchi hiyo ifikie makubaliano ya programu mpya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama tawala cha PASTEF.
Chama cha PASTEF kilitaja sababu kadhaa za uamuzi huo, zikiwemo ukosefu wa uwazi katika bajeti, hatua zisizo na ufanisi za kukabiliana na gharama za maisha, pamoja na kukataa kwa serikali kuwasilisha nyaraka muhimu au kupanga upya matumizi ya mifuko maalum.
Jumanne iliyopita, kamati ya fedha ya Bunge la Kitaifa la Senegal ilitangaza kuwa ingeipitia upya bajeti hiyo iliyorekebishwa, ambayo awali ilikuwa imeikataa.
Mkwamo huu unaweza kuvuruga matumaini ya Senegal ya kupata kura ya bodi ya IMF, mapema mwezi ujao, kuhusu programu ya miaka mitatu yenye thamani ya dola bilioni 2.2 za Marekani.
Kwa mujibu wa takwimu za IMF, deni la Senegal lilikuwa limefikia asilimia 132 ya pato la taifa (GDP) kufikia mwishoni mwa mwaka 2024. Hali hiyo ilijitokeza baada ya serikali kugundua mikopo ya mabilioni ya dola ambayo utawala uliopita haukuiripoti ipasavyo.
Bajeti iliyorekebishwa ya mwaka 2026 inashusha makadirio ya ukuaji halisi wa pato la taifa hadi asilimia 2.7 kutoka takriban asilimia 5, huku ikipanua nakisi ya bajeti hadi asilimia 7.6 ya pato la taifa kutoka asilimia 5.4.
Comments
0