Wamiliki wa pasipoti ya Ethiopia wanaweza kusafiri bila viza kwenda nchi 17 pekee, kwa mujibu wa takwimu zinazohusishwa na Kielelezo cha Nguvu ya Pasipoti Duniani (Global Passport Power Index) cha mwaka 2026. Hali hii inaonyesha vikwazo vinavyowakabili raia wa Ethiopia wanaotafuta fursa za kibiashara, kielimu na kitamaduni kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyonukuliwa na Passport Rank, kielelezo hicho kinaiweka Ethiopia katika nafasi ya 90 duniani, sambamba na nchi kama Somalia, Yemen, Syria na Afghanistan.
Mbali na nchi hizo 17, raia wa Ethiopia wanaweza kuingia katika nchi nyingine 33 kwa viza wanazopata wanapowasili. Hata hivyo, ni nchi tano tu wanachama wa Umoja wa Afrika, yaani Kenya, Benin, Gambia, Rwanda na Togo, zinazotajwa kuwaruhusu kuingia bila viza.
Nafasi hiyo inaakisi vikwazo ambavyo wasafiri wa Ethiopia hukutana navyo wanapotaka kuvuka mipaka. Maombi ya viza mapema, nyaraka nyingi na ucheleweshaji wa kushughulikia maombi vinaweza kufanya safari za kimataifa kuwa ngumu.
Ripoti hiyo inahusisha hadhi hiyo ya chini ya pasipoti na mchanganyiko wa hali ya kiuchumi, wasiwasi wa kiusalama na mahusiano ya kidiplomasia. Inaeleza kuwa serikali za kigeni kwa kawaida huzingatia viwango vya kipato, hatari za kiusalama na uwezekano wa watu kukaa zaidi ya muda wa viza zao wakati wa kuweka masharti ya kuingia.
Pia, ukosefu wa utulivu na hofu za kiusalama katika ukanda wa Pembe ya Afrika vinatajwa kuchangia ukaguzi mkali wa viza kwa wasafiri wa Ethiopia. Ripoti inaongeza kuwa mikataba michache ya kuondoleana viza kati ya nchi ni kikwazo kingine kwa uhuru wa kusafiri.
Vikwazo hivi vinaweza kuathiri wafanyabiashara wanaotaka kuhudhuria maonyesho ya biashara, kujadiliana mikataba au kujenga ushirikiano nje ya nchi. Kampuni za Ethiopia zinazotaka kupanuka kimataifa pia zinaweza kukutana na changamoto, hasa pale ambapo wafanyabiashara wa kigeni huingia Ethiopia kwa viza za kielektroniki (e-visa) au viza wanazopata wanapowasili, ilhali raia wa Ethiopia hulazimika kupitia taratibu ngumu zaidi za viza ili kutembelea masoko yanayolengwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, athari hizi zinavuka sekta ya biashara na kugusa ushirikiano wa kitaaluma, mabadilishano ya kitamaduni na ushiriki wa kimataifa kwa ujumla. Wanafunzi na watafiti wanaofuatilia programu za kubadilishana kitaaluma na fursa nyingine za kimataifa nao wanaathirika.
Comments
0