Naibu mkuu wa jeshi la polisi nchini Afrika Kusini, Luteni Jenerali Shadrack Sibiya, amejiuzulu wadhifa wake, ikiwa ni wiki tatu tangu afunguliwe mashtaka ya makosa ya kingono.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, wakili wa Sibiya aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu Jumatatu wakati wa kikao cha kinidhamu dhidi yake.
Msemaji huyo, Athlenda Mathe, aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa X kuwa kuondoka kwake katika jeshi la polisi kunahesabiwa kama kufukuzwa kazi kwa aibu.
Mashtaka hayo yanatokana na madai kwamba alimrubuni kingono msichana wa miaka 16 na kumbaka mwanamke wa miaka 18. Aidha, anakabiliwa na shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu.
Sibiya amekana mashtaka yote dhidi yake. Anakiri kuwa alifanya ngono na mwanamke huyo wa miaka 18, lakini anasisitiza kuwa ilikuwa kwa ridhaa ya pande zote mbili.
Tangu akamatwe wiki tatu zilizopita, amekuwa akishikiliwa rumande baada ya ombi lake la dhamana kukataliwa.
Kesi hii inaibuka wakati jeshi la polisi likimulikwa katika uchunguzi mkubwa wa umma kuhusu tuhuma za rushwa na kushirikiana na wahalifu.
Uchunguzi huo, unaojulikana kama Tume ya Madlanga, ulianza Septemba 2025. Tume hiyo imesikiliza tuhuma kwamba Sibiya alipokea zawadi ya swala aina ya impala 20 kutoka kwa mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu, ili kumpatia mkataba wa polisi.
Comments
0