Bondia wa Algeria Imane Khelif anatarajiwa kupanda ulingoni kwa mara ya kwanza tangu ashinde medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka 2024, baada ya waandaaji kuthibitisha Jumanne kwamba pambano lake la Desemba 15 litafanyika licha ya mpinzani wake, Clarida Sarabia, kujiondoa.
Khelif alipangiwa kuzichapa na bondia wa Uholanzi, Sarabia, mwenye umri wa miaka 21, katika pambano la kulipwa la raundi sita jijini Paris.
Msemaji wa kampuni ya uandaaji Stair Event aliiambia Reuters: “Mpinzani alilazimika kujiondoa kwenye pambano kwa sababu za kiutawala. Lakini pambano bado limepangwa kufanyika Desemba 15. Tutamtangaza mpinzani hivi karibuni.”
Kampuni inayomsimamia Sarabia, Sube La Mano Promotions, ilieleza kuwa uamuzi wa kujiondoa ulifikiwa baada ya kutafakari kwa makini mazingira yaliyopo na maslahi yake ya kitaaluma. Msemaji wake alisema: “Kwa heshima ya mwandaaji na pande zote zinazohusika, tunapendelea kuweka siri undani wa mazungumzo yetu ya faragha.”
Msemaji huyo aliongeza: “Clarida alikuwa akilisubiri kwa hamu fursa hii, na bado tuko tayari kufanikisha pambano hili siku zijazo.”
Khelif hajashiriki mashindano yoyote rasmi tangu atwae ubingwa wa uzito wa welter kwa wanawake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris, huku kukiwa na mzozo kuhusu jinsia yake na uhalali wake wa kushiriki. Mwezi Februari, alisema yuko tayari kufanyiwa kipimo cha vinasaba (genetic testing) iwapo tu kitasimamiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).
Comments
0