Watu sita, wakiwemo watoto wawili, wamepoteza maisha baada ya ndege ndogo kuanguka katika Ghuba ya Mexico, karibu na pwani ya jimbo la Mississippi nchini Marekani.
Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Marekani (US Coast Guard) kilisema wapiga mbizi waliopoa miili ya watu wazima wanne na wavulana wawili, wenye umri wa miaka minane na 10, kutoka kwenye mabaki ya ndege aina ya Cessna 210. Ndege hiyo ilianguka kati ya Pascagoula, Mississippi, na Kisiwa cha Horn, ambacho ni sehemu ya Hifadhi ya Kitaifa ya Pwani ya Gulf Islands.
Kwa mujibu wa msemaji wa Coast Guard, Juan Ros, waongozaji wa safari za ndege katika mnara wa kikanda wa Mobile, Alabama, walipoteza mawasiliano na ndege hiyo takriban saa 9:45 alasiri (3:45 p.m.) siku ya Jumanne. Tovuti ya kufuatilia safari za ndege, FlightAware, ilieleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitoka New Orleans kuelekea Fort Myers, Florida.
Timu za uokoaji zilipekua eneo hilo kwa saa kadhaa, na awali zilipata maboya matatu ya kuokolea maisha, boti ya kuokolea na sehemu ya ndani ya ndege ikielea juu ya maji.
Mratibu wa utafutaji na uokoaji wa Coast Guard katika eneo la Mobile, Kamanda Trevor Blount, aliliita tukio hilo la kuhuzunisha. “Ingawa haya si matokeo ambayo yeyote kati yetu alitarajia, tunashukuru kwa ushirikiano imara kati ya taasisi mbalimbali uliotuwezesha kuwapata haraka waliokuwa ndani ya ndege na kuzipa familia zao faraja ya kufunga ukurasa huu,” alisema.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) na Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) zitachunguza chanzo cha ajali hiyo. Tukio hili limetokea wiki chache baada ya ndege ya kibiashara aina ya Learjet 60 kuanguka Kusini mwa Florida mapema mwezi huu na kuua watu wote tisa waliokuwemo, huku ajali hiyo ikinaswa kwenye video na watu waliokuwa ndani ya magari yaliyokuwa karibu.
Comments
0