Romelu Lukaku ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kuitumikia Ubelgiji kwa miaka 16, akisema “alifurahia kila wakati” wa kuiwakilisha nchi yake.
Mshambuliaji huyo wa Fenerbahce mwenye umri wa miaka 33 alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka 2010, na anaondoka akiwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya wanaume ya Ubelgiji, akiwa na mabao 94 katika mechi 135.
Pia ni mfungaji wa tano kwa mabao mengi zaidi katika historia ya soka la kimataifa la wanaume, nyuma ya Sunil Chhetri, Ali Daei, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wa Ureno, anayeongoza orodha hiyo akiwa na mabao 146.
Lukaku alifunga mabao manane katika Kombe la Dunia mara nne alizoshiriki, ikiwemo katika safari ya Ubelgiji hadi robo fainali kwenye mashindano ya majira ya joto ya mwaka huu. Aidha, alifunga mabao sita katika michuano mitatu ya Mataifa ya Ulaya (European Championship).
Mwaka 2023, Lukaku alifunga mabao 14 katika mechi nane za kufuzu Euro 2024 akiwa na Ubelgiji, na kuweka rekodi ya mabao mengi zaidi kufungwa na mchezaji mmoja katika kampeni moja ya kufuzu michuano ya Ulaya.
Kupitia taarifa aliyoichapisha kwenye Instagram, mshambuliaji huyo wa zamani wa Everton, Chelsea na Manchester United aliwashukuru wachezaji wenzake na makocha wake “kwa kunisukuma na kuniamini ili niisaidie timu” katika kipindi chote cha maisha yake ya soka la kimataifa.
“Katika miaka hii 16 nilitoa kila nilichokuwa nacho kwa timu ya taifa… Nilipitia kila hisia inayowezekana,” Lukaku aliandika.
“Kwa mashabiki wa Ubelgiji, asanteni kwa sapoti mliyoipa timu yetu. Ninajivunia kuiwakilisha nchi yangu katika Kombe la Dunia mara nne na michuano mitatu ya Ulaya.
“Sitasahau kamwe nyakati hizo. Niko na amani na uamuzi wangu wa kuishia hapa. Ilikuwa ya ajabu. Ilikuwa ya kufurahisha. Nina shukrani.”
Lukaku alikosa ushindi wa Ubelgiji dhidi ya Uturuki katika michuano ya Nations League wiki iliyopita kutokana na jeraha la nyonga. Pia alikaa benchi bila kuingia uwanjani Jumapili, wakati Ubelgiji ilipoichapa Italia mabao 4-1 na kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Mchezaji mwenzake wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne, naye alimpongeza mshambuliaji huyo kwa kuweka picha yao wakiwa pamoja kwenye Instagram.
“Hakuna maneno ya kuelezea maana yako kwangu na kwa nchi yetu!” De Bruyne aliandika.
Comments
0