Winga wa Paris St-Germain, Khvicha Kvaratskhelia, atafanyiwa upasuaji wa goti baada ya kuchanika kano ya mbele ya goti, inayojulikana kama anterior cruciate ligament (ACL), wakati wa ushindi wa timu yake wa mabao 4-2 dhidi ya Barcelona siku ya Jumanne.
Kvaratskhelia aliumia katika purukushani na Xavi Espart, na hakuweza kukanyaga kwa mguu wake wa kulia alipokuwa akitolewa uwanjani katika dakika ya 59 ya mchezo huo wa Champions League.
Hadi sasa, PSG haijatangaza ni lini mchezaji huyo anatarajiwa kurejea uwanjani.
Kupitia taarifa aliyoiweka kwenye Instagram, Kvaratskhelia alisema: “Kabla ya kila mchezo ninaocheza humwomba Mungu niondoke uwanjani nikiwa mzima, lakini ilikuwa bure.
“Huenda nilijiandaa kwa mchezo huu kuliko nilivyowahi kujiandaa hapo awali. Nilidhani nilikuwa nimejiandaa kwa kila kitu.
“Ninatambua kuwa Mungu alinichagua, na ikiwa niliwalinda wachezaji katika uwanja mwingine, niko tayari kupitia miezi hii ya kazi ngumu, maumivu na machozi.
“Ninajua lazima nirudi nikiwa na nguvu zaidi kwa ajili ya watu wangu ambao daima wako nyuma yangu. Sitawaangusha, ninaahidi, sitapoteza hata sekunde moja.”
Kvaratskhelia, mwenye umri wa miaka 25, alihamia mji mkuu wa Ufaransa akitokea Napoli mwezi Januari 2025, na tangu hapo amesaidia PSG kutwaa mataji mawili mfululizo ya Champions League.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Georgia amecheza mechi 11 akiwa na PSG msimu huu.
Mbali na Kvaratskhelia, klabu hiyo ilithibitisha kuwa Ousmane Dembele na Marquinhos watakosekana kwa “wiki chache.” Dembele alitoka uwanjani akichechemea kutokana na jeraha la paja la kushoto, huku Marquinhos akiumia paja la kulia.
Katika uwanja wa Parc des Princes, PSG na Barcelona walikuwa sare ya mabao 2-2 zikiwa zimebaki dakika 10 za mwisho, kabla ya wenyeji kufunga mabao mawili ya kuchelewa na kuendeleza mwanzo wao wa ushindi katika kutetea taji la Champions League.
PSG sasa wanaongoza msimamo wa kundi wakiwa wameshinda mechi zote tatu walizocheza.
Comments
0