Shirika la afya ya umma la Afrika limeanzisha programu ya majaribio ya mafunzo kwa wataalamu wa afya walio katikati ya taaluma zao, kwa lengo la kuongeza uwezo wa bara hili kufanya majaribio ya kitabibu (clinical trials) na kutengeneza chanjo, dawa na vifaa vya uchunguzi wa magonjwa.
Programu hiyo ya Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) inaunganisha masomo ya kitaaluma na mafunzo kwa vitendo katika taasisi za utafiti wa kitabibu katika nchi nne za Afrika. Lengo ni kujenga kundi la watafiti wenye uwezo wa kuongoza tafiti na kusaidia juhudi za kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, “Programu hii inalenga kupanua kundi la watafiti wa Afrika wanaoweza kuongoza tafiti za kitabibu na kuchangia katika utengenezaji wa chanjo, tiba na vipimo vya uchunguzi, ikiwemo utafiti na maendeleo kwa ajili ya milipuko.”
Ikisimamiwa na Kitengo cha Sayansi na Ubunifu cha Africa CDC, programu hiyo ya cheti itaanza kwa wiki mbili za masomo ya kitaaluma mjini Addis Ababa, Ethiopia. Baada ya hapo, washiriki watapelekwa kwa mafunzo ya vitendo ya wiki nane nchini Nigeria, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia.
Masomo ya kitaaluma yatatolewa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen (AHRI) pamoja na Kituo cha Ubunifu wa Utengenezaji wa Dawa na Majaribio ya Tiba kwa Afrika (CDT-Africa), huku mashirika washirika yaliyochaguliwa yakitoa uzoefu wa utafiti kwa vitendo.
Mafunzo haya yanawalenga madaktari, wafamasia na wataalamu wengine wanaotaka ujuzi maalum katika utafiti wa kitabibu na utafiti tafsiri (translational research), maeneo muhimu katika kupima ufanisi wa afua za kitabibu na kugeuza ugunduzi wa kisayansi kuwa tiba halisi.
Mtaala unajumuisha utekelezaji wa majaribio ya kitabibu, maadili ya utafiti, usimamizi wa data, ufuatiliaji wa usalama wa dawa (pharmacovigilance), utafiti wa maabara na utafiti tafsiri, uandishi wa kisayansi pamoja na uandaaji wa maombi ya ruzuku.
Africa CDC inalenga kuimarisha uwezo wa bara hili kubuni, kuendesha na kusimamia tafiti za kitabibu, zikiwemo tafiti za kutengeneza chanjo, tiba na vipimo vinavyohitajika wakati wa milipuko ya magonjwa.
Hatua hii inakuja wakati Afrika ikihitaji kuimarisha nguvu kazi yake ya utafiti wa afya na kupanua uwezo wa ndani wa kuzalisha ushahidi kuhusu afua za kitabibu zinazoendana na vipaumbele vyake vya afya ya umma. Shirika hilo linaiona programu hii kama sehemu ya juhudi za kujenga kundi imara la watafiti wa Kiafrika watakaochangia ubunifu wa kitabibu na kuboresha utayari kwa dharura za afya zijazo.
Comments
0