Muungano wa kimataifa wa chanjo, Gavi, umetangaza Ijumaa kuwa utarejesha sehemu kubwa ya ufadhili kwa nchi zinazotaka kununua chanjo ya malaria.
Gavi inapanga kutumia msaada wa dola milioni 214 za Marekani kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ya GiveWell na Coefficient Giving kufanikisha hatua hiyo. Hii inakuja baada ya muungano huo kupunguza bajeti yake ya chanjo za malaria mapema mwaka huu, kufuatia kushindwa kufikia lengo lake la kukusanya fedha.
Gavi ni muungano wa kimataifa unaosaidia nchi maskini zaidi duniani kununua chanjo.
Akizungumza na Reuters, Mkurugenzi Mtendaji wa Gavi, Sania Nishtar, alisema kurejeshwa kwa sehemu ya fedha hizo kutamaanisha kuwa nchi hazitalazimika kupunguza utoaji wa chanjo ya malaria. Aliongeza kuwa hiyo ni hatua chanya, kwa kuwa mahitaji ya chanjo hiyo ni makubwa.
Takwimu mpya kutoka Taasisi ya Chanjo ya Sabin (Sabin Vaccine Institute) zinaonyesha kuwa nchi zenye uzoefu wa mwaka mmoja wa kutoa chanjo hiyo zimefikia wastani wa asilimia 80 ya walengwa kwa dozi ya kwanza na asilimia 70 kwa dozi ya tatu. Chanjo hiyo inahitaji dozi nne ili kutoa kinga kamili, huku dozi ya mwisho ikitolewa mtoto anapokuwa katika mwaka wake wa pili wa maisha.
Malaria huua zaidi ya watu 500,000 kila mwaka, wengi wao wakiwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wataalamu wanasema chanjo hiyo, ikiambatana na mbinu nyingine za kukabiliana na ugonjwa huo, imeanza kuleta matokeo.
“Tunashuhudia kupungua kwa kasi kwa visa vya malaria, na akina mama wanaliona hilo,” alisema Eric Nebie, mkuu wa mpango wa utekelezaji wa chanjo ya malaria wa shirika la PATH, unaosaidia nchi zinazoanzisha chanjo hiyo, zikiwemo Uganda na Burkina Faso.
Awali, Gavi ilikuwa ikigharamia hadi asilimia 85 ya mahitaji yaliyokadiriwa ya chanjo katika maeneo yenye viwango vya juu na vya kati vya maambukizi ya malaria. Kama Reuters ilivyoripoti Januari 2026, kiwango hicho kilishushwa hadi asilimia 70 kwa maeneo yanayoagiza chanjo kwa mara ya kwanza.
“Hili lilisababisha wasiwasi mkubwa; mawaziri wengi walipiga simu,” alisema Nishtar. “Kwa hiyo tulienda kutafuta fedha ili tusilazimike kukishusha.”
Alisema kwamba kwa msaada huo wa GiveWell, Gavi itaweza kurejesha ufadhili hadi asilimia 85.
Katika hatua nyingine, Gavi inatarajiwa kutoa malipo ya kwanza kupitia mpango wake wa Kuharakisha Utengenezaji wa Chanjo Afrika (African Vaccine Manufacturing Accelerator), unaolenga kuongeza uzalishaji wa chanjo kote barani.
Muungano huo utatoa hadi dola milioni 30 za Marekani kusaidia Taasisi ya Pasteur (Institut Pasteur) iliyoko Dakar, Senegal, kwa kazi yake kuhusu chanjo ya homa ya manjano.
Comments
0