Uganda inatarajiwa kupokea shehena yake ya kwanza ya toleo nafuu la sindano mpya ya kimapinduzi ya kuzuia virusi vya UKIMWI (VVU), hatua inayoongeza matumaini ya kupanua upatikanaji wa dawa hiyo barani Afrika, ambako mzigo wa ugonjwa huo bado ni mkubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Dunia (Global Fund), shehena ya kwanza duniani ya dawa hiyo ya jenetiki (generic), inayojulikana kama lenacapavir, iliwasili Zambia siku ya Jumatano, na Uganda inatarajiwa kupokea yake katika siku chache zijazo.
Zimbabwe inatarajiwa kupokea dawa hiyo mapema mwaka ujao, na nchi nyingine kadhaa zitafuata.
Dawa hiyo hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili kwa mwaka, ina ufanisi wa karibu asilimia 100 katika kuzuia maambukizi ya VVU, na gharama yake inatarajiwa kuwa dola 40 tu za Marekani kwa mtu mmoja kwa mwaka.
Ujio wa dawa hii ya jenetiki unakuja mwaka mmoja tu baada ya toleo la awali, lililotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Marekani, Gilead Sciences, kuanza kupatikana katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Toleo hilo la awali liligharimu takriban dola 28,000 za Marekani kwa mwaka nchini Marekani, kiasi ambacho kiliwaweka watu wengi katika nchi zinazoendelea nje ya uwezo wa kuipata.
Lenacapavir hushambulia ganda la protini linalolinda VVU, na hivyo kuvuruga uwezo wa virusi hivyo kujizalisha na kuanzisha maambukizi mwilini.
Katika jaribio la kihistoria la kitabibu lililofanyika mwaka 2024 nchini Uganda na Afrika Kusini, likiwahusisha zaidi ya wasichana balehe na wanawake vijana 5,000, hakuna hata mmoja kati ya waliopokea sindano hiyo aliyeambukizwa VVU.
Wataalamu wa afya wanasema sindano hiyo ina faida kubwa ikilinganishwa na vidonge vilivyopo vya kuzuia VVU, vinavyojulikana kama PrEP (pre-exposure prophylaxis), ambavyo lazima vimezwe kila siku na vinaweza kuambatana na unyanyapaa. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza dawa hiyo kwa ajili ya kuzuia VVU mwezi Julai 2025.
Mfuko wa Dunia ulieleza kuwasili kwa dawa hiyo barani Afrika kuwa “mafanikio makubwa” katika mapambano dhidi ya VVU, ukisema kuwa upatikanaji wa dawa nafuu utasaidia kuwafikia mamilioni zaidi ya watu walio hatarini kuambukizwa.
“Shehena hizi zinaashiria kasi na upanuzi usio na kifani katika upatikanaji wa dawa ya jenetiki ya kuzuia VVU yenye ufanisi mkubwa na ubora uliothibitishwa, katika mazingira ya kipato cha chini na cha kati,” shirika hilo lilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Dunia, zaidi ya watu 189,000 katika nchi 10 tayari wamepokea sindano yao ya kwanza ya lenacapavir. Shirika hilo linatarajia nchi 24 kuwa zimepokea dawa hiyo kufikia mwisho wa mwaka huu, na kwa kushirikiana na serikali ya Marekani, linapanga kuwafikia angalau watu milioni tatu kufikia mwisho wa mwaka 2028.
Hatimaye, dawa hiyo inatarajiwa kupatikana katika nchi 120 za kipato cha chini na cha kati.
Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zina karibu theluthi mbili ya watu wote wanaoishi na VVU duniani, huku wasichana balehe na wanawake vijana wakiathirika zaidi. Afrika Kusini, ambayo ni miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kupokea sindano hiyo nafuu, ina idadi kubwa zaidi duniani ya watu wenye VVU, takriban milioni nane.
Kwa mujibu wa WHO, takriban watu milioni 41 duniani kote walikuwa wakiishi na VVU mwaka jana, huku watu 570,000 wakifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na VVU.
Usambazaji huu unafanyika wakati kukiwa na wasiwasi kuwa upunguzaji mkubwa wa misaada ya nje ya Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump unaweza kuhujumu mafanikio ya miongo kadhaa katika kupambana na VVU barani Afrika, ambako nchi nyingi zinategemea sana ufadhili wa kimataifa kwa huduma za kinga na matibabu.
Umoja wa Mataifa unalenga kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
Comments
0