Leroy Boseman, baba wa marehemu Chadwick Boseman, nyota wa filamu ya Black Panther, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kifo chake kimekuja miaka sita baada ya kumpoteza mwanawe, muigizaji huyo maarufu wa Hollywood.
Kwa mujibu wa ripoti, familia ya Boseman ilitangaza msiba huo kupitia taarifa rasmi, ikimwelezea Leroy kama mume na baba mpendwa, aliyekuwa nguzo muhimu katika maisha yao.
Familia hiyo ilisisitiza kuwa nafasi yake kwao ilikuwa kubwa kuliko jinsi dunia ilivyomfahamu. “Kwa ulimwengu, yeye [Leroy] huenda akajulikana kama baba wa Derrick, Kevin na Chadwick Boseman. Kwetu sisi, alikuwa zaidi ya hapo,” ilisema familia.
Katika kipindi hiki cha maombolezo, familia imesema inatafakari maisha yake na nyakati walizoshiriki pamoja. “Tunapoomboleza kifo chake, tunatafakari kwa shukrani maisha aliyoishi, kumbukumbu tulizoshiriki na urithi anaouacha,” taarifa hiyo iliongeza.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa wanafamilia wamesimama pamoja na wanaendelea kufarijiana katika kipindi hiki cha msiba.
“Katika kipindi hiki kigumu, tunabaki wamoja kama familia, tukisaidiana na kuienzi kumbukumbu yake. Tunaomba kwa heshima faragha, huruma na uelewa wakati familia yetu ikipitia msiba huu mzito,” ilisema taarifa hiyo.
Chadwick Boseman, aliyejulikana zaidi kwa kuigiza kama T’Challa katika filamu ya Black Panther ya Marvel, alifariki dunia Agosti 2020 akiwa na umri wa miaka 43, baada ya kupambana kimyakimya na saratani ya utumbo mpana.
Comments
0