Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, pamoja na washirika wake zaidi ya kumi na wawili, wamefunguliwa mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali na kupelekwa Mahakama Kuu kujibu kesi ya uhaini. Hayo yamebainika kupitia hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani jijini Lusaka Jumatatu.
Kwa mujibu wa hati hiyo, Mundubile, mgombea mwenza wake Makebi Zulu na watu wengine 12 wanatuhumiwa kupanga njama ya kuiangusha serikali katika kipindi cha kati ya Aprili na Agosti 2026.
Hati hiyo pia inadai kuwa Mundubile na mfanyabiashara mmoja walitoa fedha za kugharamia mafunzo ya kijeshi nchini Urusi kwa watu watano, kwa lengo la kujaribu kuipindua serikali.
Mundubile, aliyegombea urais kupitia chama cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), na Zulu walikamatwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma za uhaini muda mfupi baada ya uchaguzi wa urais wa Agosti 13. Wawili hao walidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na wizi wa kura.
Rais Hakainde Hichilema, aliyeshinda muhula mwingine madarakani, amekanusha madai hayo ya udanganyifu.
Wakili wa utetezi, Sakwiba Sikota, alisema mashtaka hayo hayaleti maana yoyote na kwamba upande wa mashtaka uko kwenye “msako wa kubahatisha” (fishing expedition).
Mundubile mwenyewe amekuwa akisisitiza tangu awali kuwa hana hatia na kwamba mashtaka dhidi yake yamechochewa na siasa.
Kwa mujibu wa Sikota, kesi hiyo inatarajiwa kuanza mapema mwaka ujao.
Wachambuzi na waangalizi wamesema uchaguzi wa Agosti uligubikwa na kasoro kubwa, jambo lililochafua sifa ya kidemokrasia ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye utajiri mkubwa wa madini.
Comments
0