Wanamuziki maarufu wa Kenya David Mathenge, anayejulikana zaidi kama Nameless, na mkewe Wahu Kagwi wamefunguka kuhusu namna wanavyoendesha maisha ya nyumbani. Wanandoa hao, ambao wamekuwa pamoja kwenye ndoa kwa karibu miongo miwili na wana mabinti watatu, wameeleza kwa kina mpangilio wao wa kugawana kazi za nyumbani.
Kupitia video ya maswali na majibu waliyoichapisha mitandaoni, wawili hao walieleza kuhusu Mathenge Family Charter, mpango walioanzisha mapema mwaka huu kwa lengo la kugawanya upya majukumu ya nyumbani.
Kwa miaka mingi, Wahu ndiye aliyekuwa kiini cha usimamizi wa shughuli zote za nyumbani. Hata hivyo, uzito wa majukumu hayo ulijilimbikiza hadi kumsababishia uchovu mkubwa. Wahu alieleza kuwa uamuzi wa kubadilika ulikuja baada ya kuchoshwa kupita kiasi na mzigo wa kiakili (mental load) wa kuendesha nyumba.
“Mwanzoni mwa mwaka, tuliunda Mathenge Family Charter kama njia ya kuondoka kwenye nyumba inayomtegemea mama na kuhamia kwenye nyumba inayoendeshwa kwa mfumo,” Wahu alisema. “Lengo lilikuwa kupunguza mzigo wa kiakili niliokuwa nikiubeba kwa sababu yoh!!! Inaweza kuchosha sana wakati mwingine.”
Mkataba huo unaongozwa na kanuni nne zinazojulikana kama 4Rs: Kutambua kazi zisizoonekana (Recognise), Kuzigawanya kwa haki (Redistribute), Kupunguza mzigo kwa mama (Reduce), na Kutuza ushiriki wa timu (Reward).
Katika video hiyo, wanandoa hao walifafanua jinsi majukumu yanavyogawanywa chini ya mfumo huo mpya:
Kuwapeleka watoto shuleni: Wahu ndiye huwapeleka shuleni asubuhi na mapema, wakati Nameless akiwa bado amelala.
Masomo na ada za shule: Wahu husimamia kazi za nyumbani za shule, huku Nameless akilipa ada na kusaidia maswali mepesi.
Ununuzi wa mahitaji ya nyumbani: Kazi hii ilikuwa ya Wahu, lakini sasa Nameless ndiye huenda dukani, au huagiza mahitaji pamoja.
Kuwasikiliza watoto: Wahu husikiliza hadithi za kila siku za mabinti wao baada ya shule. Nameless alikiri kuwa wasichana hao huepuka kumweleza mambo yao kwa sababu yeye huwa mwepesi kutoa ushauri badala ya kusikiliza tu.
Usafi wa nyumba: Kazi za usafi hugawanywa kati ya wanafamilia na msimamizi wao wa nyumbani, Massie, hali inayopunguza mzigo kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Miadi ya matibabu: Wahu hupanga ratiba za huduma za afya kwa ajili yake, Nameless na watoto.
“Kiwango cha mafanikio??? - Ningesema tuko asilimia 25-30,” Wahu alisema, akisisitiza kuwa familia hiyo inathamini maendeleo kuliko ukamilifu. “Huwa nawaambia marafiki zangu jinsi ambavyo sasa nina RAM ya ziada ya kushiriki shughuli nyingine zinazonipa furaha.”
Kwa upande wake, Nameless alisema kutambua uzito wa kazi za nyumbani kumeboresha hali ya maisha yao na akawahimiza wanaume wengine kutathmini kazi zisizoonekana katika nyumba zao. “Kwa kweli nadhani kuelewa kazi zisizoonekana kumeleta maelewano zaidi nyumbani,” alisema Nameless. “Ningependekeza kwa jamaa zangu wote huko nje.”
Comments
0