Mwimbaji wa Kenya, Otile Brown, ameeleza wasiwasi wake kuhusu kushuka kwa ubora wa muziki wa kisasa, akisema nyimbo nyingi za sasa hazina tena ule mvuto unaowafanya wasikilizaji kuzirudia mara kwa mara.
Kupitia ujumbe alioweka kwenye stories za mitandao ya kijamii, Otile alisema amekuwa akitafakari mwelekeo wa muziki na jinsi watu wanavyosikiliza nyimbo siku hizi. Kauli yake imezua mjadala kuhusu ubora wa muziki na iwapo nyimbo za leo zinaacha alama ya kudumu kama zile za miaka iliyopita.
Otile alisema alilazimika kuanza upya wakati akiandaa EP yake ijayo, ili kuziba pengo analoamini limekosekana katika muziki wa kisasa. Alikiri kuwa mwelekeo wake mpya huenda ukamfanya asikike kama msanii chipukizi, lakini akasisitiza kuwa kuanza upya ni muhimu ili kusonga mbele.
“Hapana, kwa EP hii ijayo, nina furaha kwa ajili ya familia yangu halisi ya muziki. Nawaahidi, hakuna wimbo wa kuruka!” aliandika.
Ahadi hiyo inaonyesha kuwa anataka kila wimbo kwenye mradi huo uwe na ubora sawa, badala ya kutegemea wimbo mmoja au miwili pekee kuubeba mradi mzima.
Hadi sasa, Otile hajatangaza tarehe ya kutoka kwa EP hiyo wala orodha ya nyimbo zake, hali inayowaacha mashabiki wakisubiri kusikia sura mpya ya muziki wake.
Otile Brown, ambaye jina lake halisi ni Jacob Obunga, amejenga jina lake kupitia muziki wa R&B na nyimbo za mapenzi. Alitoa albamu yake ya kwanza, Best of Otile Brown, mwaka 2017, ikifuatiwa na Just in Love mwaka 2020 na Grace mwaka 2024. Miongoni mwa nyimbo zake maarufu ni Chaguo la Moyo akimshirikisha Sanaipei Tande, Baby Love, Dusuma akimshirikisha Meddy, na Jeraha akimshirikisha Jovial.
Comments
0