Kenya na Rwanda zimeanza kutumia njia mpya ya kuagiza mafuta kwa wingi kupitia Ushoroba wa Kaskazini (Northern Corridor), baada ya shehena ya tani 40,000 kuwasili Mombasa Jumanne ikiwa ya kwanza chini ya mfumo huo unaoungwa mkono na serikali za nchi hizo mbili.
Mafuta hayo, yaliyobebwa na meli MT Sea Wolf, yalipokelewa katika Kituo cha Mafuta cha Kipevu 2 (KOT2) cha Kenya Pipeline Company. Hatua hiyo inafungua njia mpya kwa bidhaa za petroli zilizosafishwa za Rwanda kupitia bandari, bomba na miundombinu ya kuhifadhi mafuta ya Kenya.
Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, James Opiyo Wandayi, alisema nchi hizo mbili zinatarajia kiasi cha mafuta kinachopita kwenye ushoroba huo kuongezeka mara kumi katika miaka ijayo, jambo litakaloipa Kenya nafasi kubwa zaidi katika mnyororo wa usambazaji mafuta wa Rwanda.
“Unaimarisha nafasi yetu kama kitovu cha usafirishaji na upitishaji wa nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na ni ishara halisi ya muunganiko wa kina wa kiuchumi tunaoujenga na majirani zetu,” alisema.
Kwa Rwanda, mkataba huo unalenga kupunguza hatari ya kutegemea njia moja ya usambazaji. Waziri wa Nchi anayeshughulikia Miundombinu, Armand Zingiro, alisema nchi hiyo imelazimika kutathmini upya uimara wa mnyororo wake wa mafuta kufuatia misukosuko iliyotokana na machafuko nje ya mipaka yake.
“Rwanda ni nchi isiyo na bahari inayoagiza bidhaa zake zote za petroli, na mwaka huu umetukumbusha jinsi machafuko yaliyo mbali na mipaka yetu yanavyoweza kuhisiwa haraka kwenye pampu zetu za mafuta,” Zingiro alisema.
Aliongeza kuwa Rwanda pia inaendeleza njia nyingine kupitia Bandari ya Tanga nchini Tanzania, huku mpango wa Kenya ukiongeza chaguo jingine la kuhakikisha upatikanaji wa mafuta.
Mpango huo unatokana na Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa tarehe 29 Juni 2026 kati ya Wizara ya Nishati na Petroli ya Kenya na Wizara ya Biashara na Viwanda ya Rwanda. Unaungwa mkono na mkataba wa pande tatu unaohusisha wizara hizo mbili na Rwanda National Energy Company (RNEC), pamoja na mkataba kati ya RNEC na Kenya Pipeline Company unaosimamia usafirishaji, uhifadhi, upangaji ratiba na ushughulikiaji wa mafuta ya Rwanda.
Serikali hizo mbili zinasema mpango huo utaboresha ufanisi wa mnyororo wa usambazaji na kupunguza gharama za usafirishaji kwa sekta ya petroli ya Rwanda, huku ukiimarisha usalama wa nishati na biashara ya kikanda.
Comments
0