Baraza la mahakama (jury) nchini Marekani limeiamuru Apple kulipa fidia ya dola bilioni 5.7 za Marekani (takriban pauni bilioni 4.3 za Uingereza), baada ya kubaini kuwa kampuni hiyo ilitumia teknolojia ya kampuni nyingine bila ruhusa.
Mwaka 2021, kampuni ya vifaa vya sauti ya Taction Technology ilidai kuwa Apple ilikiuka hataza (patents) zake mbili za mifumo ya mguso (haptics), teknolojia inayowezesha mitetemo pale mtumiaji anapopokea ujumbe au kubonyeza kitufe. Teknolojia hiyo imejengwa ndani ya vifaa kama iPhone na Apple Watch.
Taction, inayotengeneza vipokea sauti vya masikioni (headphones) na vile vya michezo ya video, ilidai kuwa maboresho ya mfumo wa Apple yalikiuka hataza ilizopewa mwaka 2020. Katika hati yake ya mashtaka, ilieleza kuwa kwa kuzalisha mitetemo bora zaidi kwenye vifaa vyake, Apple iliweza kuboresha uzoefu wa jumla wa watumiaji wake.
Kwa sababu hiyo, kwa mujibu wa Taction, kampuni hiyo kubwa ya teknolojia imekuwa “ikinufaika na ubunifu na mafanikio ya Taction kwa kuuza vifaa vinavyokiuka hataza [zake]”. Taction pia iliituhumu Apple kwa kutumia uvumbuzi wake “bila leseni wala mamlaka”.
Apple ilikanusha kutumia teknolojia ya mtetemo ya Taction na kusema itakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. “Ingawa tunalishukuru baraza la mahakama kwa kulitafakari suala hili, hatukubaliani kabisa na hukumu ya leo na fidia iliyotolewa, ambazo hazina msingi wowote katika ukweli,” ilisema kampuni hiyo.
Kampuni hiyo iliongeza: “Taptic Engine ya Apple ni tofauti kimsingi na teknolojia ya Taction, jambo ambalo majaribio ya Taction yenyewe kwenye bidhaa za Apple yalithibitisha wakati wa kesi.”
Teknolojia ya haptics huwawezesha watu kuingiliana na vifaa kwa kuiga hisia ya kugusa au kuhisi kupitia mitetemo. Imekuwa alama kuu ya vifaa vya kisasa; simu janja, saa na vidhibiti vya michezo ya video ni miongoni mwa vifaa vyenye mota ndogo zinazosogea kulingana na ishara maalum za kielektroniki.
Mfumo wa Apple unaoitwa “Taptic Engine”, unaowezesha mrejesho wa mguso kwenye vifaa vyake, ulianza kutumika kwa mara ya kwanza kwenye Apple Watch mwaka 2014. Tangu wakati huo, kampuni imeuboresha mfumo huo wa msingi na kupanua matumizi ya haptics kwenye vifaa vyake.
Mwaka 2023, jaji mmoja mjini San Diego aliamua kuwa Apple haikukiuka hataza za Taction. Hata hivyo, rufaa ilishughulikiwa baadaye na mahakama ya rufaa ya shirikisho, hatua iliyopelekea kesi kusikilizwa mbele ya baraza la mahakama mwezi Septemba katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani kwa Wilaya ya Kusini ya California, ambayo iliamua kwa upande wa Taction.
Katika hukumu iliyotolewa Ijumaa, baraza hilo halikubaini kuwa Apple ilikiuka hataza hizo kwa makusudi.
Kesi hii ni mojawapo ya kesi nyingi zinazofanana ambazo kampuni hiyo kubwa ya teknolojia imelazimika kujitetea dhidi yake katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi Novemba 2025, jaji aliiamuru Apple kulipa dola milioni 634 za Marekani kwa kampuni ya teknolojia ya matibabu Masimo, baada ya baraza la mahakama kubaini kuwa ilikiuka hataza ya teknolojia ya kupima kiwango cha oksijeni kwenye damu.
Comments
0