China inapanua kwa kasi vituo vya kuhifadhi data, inakuza wataalamu na kuendeleza teknolojia ya akili bandia (AI), wakati Beijing na Washington zikiwania kutawala sekta hiyo muhimu.
Katika mbuga za nyasi za Mongolia ya Ndani, wakulima wa viazi sasa wanaishi bega kwa bega na sekta ya kidijitali inayokua kwa kasi. Mjini Ulanqab, unaojulikana kama “mji mkuu wa viazi” wa China, majengo makubwa ya vituo vya data yanachipuka kila upande huku Beijing ikiharakisha malengo yake ya akili bandia.
Mamia ya wafanyakazi wako kazini wakijenga vituo vipya, huku winchi zikinyanyua vifaa na makundi ya ujenzi yakiendelea na awamu moja baada ya nyingine za miradi hiyo. “Hii ndiyo kasi ya China,” mfanyakazi mmoja alisema kwa utani.
Miundombinu hii ni nguzo kuu ya juhudi za China za kusambaza AI katika uchumi na jamii nzima. Beijing inalenga kuingiza akili bandia katika asilimia 90 ya viwanda na maeneo ya jamii ifikapo mwaka 2030. Upanuzi huu pia unaisaidia China kujenga kundi kubwa zaidi la wahandisi na watafiti wa AI.
Jack Zhang wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha China alirudi nchini baada ya kusoma katika vyuo vikuu vya Yale na Cambridge.
“Nilitaka kuchukua sehemu ya kazi ya AI niliyokuwa nikiifanya maabara na kuitumia katika afya na tiba ya binadamu,” alisema. “Hilo linahitaji rasilimali zaidi, watu zaidi na wakati mwingine msaada zaidi wa serikali, jambo ambalo linaweza kuwa gumu kupatikana ughaibuni.”
Kwa mujibu wa Zhang, idadi ya wanafunzi na watafiti wa Kichina wanaohamia Marekani inapungua, huku wengi zaidi wakirejea China. Uwezo huu unaokua wa China katika AI ni kipengele kikubwa katika ushindani wa kiteknolojia kati yake na Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema, “Anayeshinda AI, ndiye mshindi,” wakati mtendaji mkuu wa Anthropic, Dario Amodei, amesisitiza kuwa Washington inapaswa kuendeleza vikwazo vya uuzaji wa chipu za kisasa na vifaa vyake kwa China. Amodei pia ametahadharisha kuwa China ikiongoza katika AI kunaweza kuleta hatari kubwa kwa Marekani na dunia kwa ujumla.
Beijing imepinga hofu hizo. Gazeti la serikali la Global Times lilielezea juhudi za Marekani za kudhibiti maendeleo ya AI ya China kuwa sehemu ya “mbinu za Vita Baridi” zinazolenga kuzuia kuinuka kwa taifa hilo.
China pia inanadi mtazamo tofauti wa kuendeleza AI. Rais Xi Jinping amehimiza kampuni za Kichina kutengeneza mifumo ya bei nafuu ya chanzo huria (open-source), inayowaruhusu watumiaji, biashara na mataifa kuirekebisha teknolojia hiyo. Hii ni tofauti na mifumo iliyofungwa ya kampuni kama OpenAI na Anthropic, ambazo misingi ya muundo wake haiko wazi kwa umma.
Kampuni za Kichina zimetumia mfumo huo wa wazi kubadilishana teknolojia na kuharakisha ubunifu, na pia kukwepa vikwazo vya kupata chipu za kisasa za kompyuta. Beijing inataka sauti kubwa zaidi katika kuandaa kanuni za kimataifa za AI, na Xi amekuwa akitoa wito mara kwa mara wa udhibiti madhubuti na mfumo wa kimataifa wa kusimamia teknolojia hiyo — hali inayoweka usalama na udhibiti wa AI katikati ya mazungumzo kati ya Washington na Beijing.
Hata hivyo, kasi ya upanuzi wa China haionyeshi dalili ya kupungua. Mamia ya vituo vya data yanajengwa au kupanuliwa katika maeneo kama Ulanqab, Ningxia, Gansu na Guizhou kwa ajili ya kampuni zikiwemo Huawei, ByteDance na DeepSeek. Maeneo hayo yana ardhi ya bei nafuu, hali ya hewa ya baridi na vyanzo vingi vya nishati jadidifu, huku nishati ya upepo na jua ikiongezeka kwa kasi na kupunguza gharama na mahitaji ya nishati ya kuendesha vituo hivyo.
Lakini kuna pia wasiwasi wa kimazingira na kijamii. China inataka vituo vyake vingi vya data viendeshwe kwa nishati safi ifikapo mwaka 2030, lakini sehemu za gridi ya umeme bado zinategemea makaa ya mawe, na upatikanaji wa maji ni changamoto nyingine katika maeneo kame ya Mongolia ya Ndani. Baadhi ya vijiji vimehamishwa ili kupisha maendeleo, ingawa ukubwa wa uhamishaji huo na fidia waliyopewa wakazi bado ni vigumu kuthibitisha.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, aliyezungumza bila kutaka jina lake litajwe, alihoji faida za vituo hivyo. “Data hizi kubwa hazina uhusiano wowote kabisa na watu wa kawaida,” alisema. “Zimetuletea faida gani?” Baadhi ya wakazi walisema wamepata ajira chache katika vituo hivyo, na wakaonyesha hofu kwamba maendeleo zaidi yanaweza kutishia mashamba yao.
Wengine wanaliona suala hili kwa jicho tofauti. Mwanamume mmoja wa eneo hilo aliyetambulishwa kwa jina lake la ukoo, Zhang, alisema watoto wake wamepata kazi zinazohusiana na maendeleo hayo mapya. “China sasa iko mstari wa mbele duniani,” alisema.
China pia inazalisha wahitimu wengi zaidi wa sayansi na teknolojia kuliko Marekani, hali inayojenga msingi mpana wa watafiti na watengenezaji wa AI wa baadaye. Dang Ronghao, mtengenezaji wa AI mwenye umri wa miaka 27 anayefanya kazi katika kampuni kubwa ya teknolojia, alisema watafiti wa Kichina wanazidi kuunganisha AI na nyanja kama muunganiko wa nyuklia (nuclear fusion), elimu ya anga, malighafi mpya na utengenezaji wa dawa. “Nadhani tunaingia katika zama nzuri,” alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wasomi wanasema mazingira ya utafiti nchini China bado hayako wazi kama wangetaka. Profesa Liu Jun wa Idara ya Takwimu na Sayansi ya Data katika Chuo Kikuu cha Tsinghua, ambaye pia amefundisha Harvard na Stanford, alisema huwahimiza wanafunzi kupinga mawazo mara nyingi zaidi.
“Si wazi kama ninavyotamani,” alisema. “Ninaendelea kuwahimiza wanafunzi hapa kuuliza maswali zaidi, kupinga zaidi, lakini hilo ni gumu kubadilika. Nadhani kwa sehemu ni utamaduni, na kwa sehemu ni mfumo.”
Nje ya vitovu vya teknolojia vya China, watu wengi bado wanashughulishwa zaidi na shinikizo za kiuchumi kama ukuaji hafifu, ukosefu wa ajira kwa vijana na kushuka kwa bei za nyumba. Katika maeneo ya vijijini ya Mongolia ya Ndani, baadhi ya wakulima wanasema kukua kwa AI kumeleta tofauti ndogo katika maisha yao.
“Data kubwa na mambo hayo yote ni mazuri, lakini hayanihusu mimi,” mkulima mmoja alisema huku akikagua kondoo wake. Alisema hutumia intaneti mara chache na ameona mabadiliko kidogo katika maisha yake ya kila siku. “Kwa kweli hakujakuwa na mabadiliko yoyote kwangu. Sijui kuhusu siku zijazo,” alisema.
Pengo hili kati ya malengo makubwa ya kiteknolojia ya Beijing na uzoefu wa watu wa kawaida linaweza kuwa changamoto kubwa wakati China ikisonga mbele kuelekea uchumi unaotegemea zaidi akili bandia.
Comments
0