Kenya itautumia Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Serikali za Jumuiya ya Madola (CHOGM) kushinikiza mageuzi katika mfumo wa fedha wa kimataifa, pamoja na upatikanaji wa haki wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei, amesema Kenya itasimamia maslahi ya Afrika katika majadiliano kuhusu maendeleo endelevu, ufadhili wa masuala ya tabianchi na mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa.
Sing’oei, ambaye tayari amewasili Antigua na Barbuda kabla ya mkutano huo utakaofanyika kuanzia Novemba 1 hadi 4, alieleza kuwa ushiriki wa Kenya utajikita katika kupata ushirikiano utakaounga mkono vipaumbele vya maendeleo vya nchi hiyo.
Naibu Rais Kithure Kindiki ataongoza ujumbe wa Kenya na kumwakilisha Rais William Ruto katika mkutano huo unaofanyika mjini St. John’s.
Serikali pia inalenga kutafuta fursa za kukuza ujuzi, ujasiriamali na fursa za kidijitali, hasa kwa vijana na wanawake. Aidha, Kenya inatarajiwa kutumia mikutano ya kibiashara na ya uwekezaji itakayofanyika pembeni mwa mkutano huo kutangaza miradi katika sekta za miundombinu, nishati, utalii, teknolojia na uchumi wa buluu.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu “Kuharakisha Ushirikiano na Uwekezaji kwa Jumuiya ya Madola Yenye Ustawi,” unawakutanisha viongozi kutoka nchi wanachama 56 zenye jumla ya takriban watu bilioni 2.7.
Comments
0