Benki ya Afrika ya Uagizaji na Uuzaji Nje (Afreximbank) na Shirika la Nchi za Afrika Zinazozalisha Mafuta (APPO) zimeanzisha rasmi Benki ya Nishati ya Afrika (Africa Energy Bank), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afreximbank siku ya Jumamosi.
Benki hiyo, ambayo ina mtaji ulioidhinishwa wa dola bilioni 5 za Marekani, inalenga kuziba pengo la ufadhili linalojitokeza wakati wakopeshaji wa jadi wakijiondoa katika kufadhili nishati ya mafuta ya visukuku (fossil fuels). Hata hivyo, mafuta na gesi bado ni nguzo kuu ya mifumo ya nishati barani Afrika.
Katika mkutano mkuu wa kwanza wa benki hiyo uliofanyika Abuja, Nigeria, Helmy Ghazi aliteuliwa kuwa rais wake wa kwanza, na bodi ya kwanza ya wakurugenzi iliundwa.
Benki hiyo itaunga mkono miradi katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya nishati, kuanzia utafutaji na uzalishaji hadi usafishaji na usambazaji.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, mahitaji ya uwekezaji katika sekta ya nishati barani Afrika yanakadiriwa kufikia dola bilioni 200 za Marekani. Awali, iliripotiwa kuwa benki hiyo ingelenga kujenga rasilimali (asset base) zenye thamani ya dola bilioni 120.
Mnamo Februari 2025, ripoti zilieleza kuwa benki hiyo ilikuwa ikilenga kuzinduliwa katikati ya mwaka 2025, huku Afrika Kusini ikionyesha nia ya kujiunga licha ya kutokuwa mwanachama wa APPO.
Comments
0