Mwandishi wa Canada mwenye asili ya Haiti, Thélyson Orélien, amekanusha madai kwamba akili bandia (AI) ilitumika kuandika riwaya yake iliyoshinda tuzo, C’était ça ou mourir.
Utata huu umeibuka muda mfupi baada ya riwaya hiyo kushinda tuzo ya Prix du Roman Fnac, tuzo kubwa ya kwanza ya msimu wa fasihi nchini Ufaransa. Orélien, mwenye umri wa miaka 38, pia yumo kwenye orodha ya mwisho ya wanaowania tuzo za Goncourt na Renaudot, mbili kati ya tuzo za fasihi zinazoheshimika zaidi nchini Ufaransa.
Kundi moja la Ufaransa linalojulikana kama Balance ton Claude limedai kuwa riwaya hiyo iliandikwa “karibu kabisa” na AI.
Katika chapisho la hivi karibuni kwenye mtandao wa X, kundi hilo lilisema lilijaribu vifungu kadhaa vya muswada huo kwa kutumia Pangram, zana ya kubaini maandishi ya AI ambayo lilieleza kuwa ndiyo “sahihi zaidi kwa mbali.”
Kwa mujibu wa kundi hilo, vifungu kadhaa vilivyojaribiwa vilionyesha matokeo ya asilimia 100 ya AI. Kundi hilo pia lilitaja kile lilichokieleza kuwa kiwango cha Pangram cha kutoa majibu ya uongo ya AI (false-positive) cha asilimia 0.0041.
Kundi la Balance ton Claude lilihoji iwapo Orélien alipaswa kuitambua AI kama mwandishi mwenza, likisema: “Je, isingekuwa uaminifu zaidi kwa mwandishi kumtaja mwandishi mwenzake?”
Hata hivyo, Orélien alikanusha madai hayo katika mahojiano na gazeti la Ufaransa, Libération, akisema hakutumia AI kuandika kitabu hicho.
“Siku zote nimependa ubunifu na fasihi. Sioni kwa nini nijisikie kulazimika kutumia mashine,” alisema.
Mwandishi huyo pia alisema kazi hiyo inaakisi mila zake za Haiti na Karibiani, akieleza kuwa taswira, marudio na midundo iliyomo ni yake mwenyewe.
Mchapishaji wake, Grasset, naye alimtetea, akiyaeleza madai hayo kuwa “yanadhuru kwa kiwango cha kutisha” mwandishi mwenye historia ya maisha ya kipekee, na kuiita kazi hiyo “halisi na yenye nguvu.”
C’était ça ou mourir inasimulia kisa cha mwalimu anayekimbia ghasia za magenge nchini Haiti kabla ya hatimaye kufika Canada, ambako anaanza maisha mapya.
Orélien alizaliwa mwaka 1988 mjini Gonaïves, kaskazini mwa Haiti, na baadaye alihamia Montreal, Canada, ambako alifanya kazi kama mwandishi wa habari. Kazi zake za awali za fasihi zilikuwa hasa maandishi ya kishairi.
Comments
0