Austria, Ujerumani, Uholanzi, Denmark na Ugiriki zimeanza mara moja mazungumzo na Rwanda yenye lengo la kuanzisha nchini humo kituo cha kuwahamishia wahamiaji (deportation hub) chini ya mfumo mpya wa Umoja wa Ulaya (EU), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Austria siku ya Jumatatu.
Nchi hizo tano wanachama wa EU zimeamua kuendesha mazungumzo hayo kwa pamoja, zikitumia mfumo mpya ulioandaliwa na umoja huo. Taarifa ya serikali ya Austria ilieleza kuwa hatua hiyo inaanza bila kuchelewa.
Tarehe 16 Novemba 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria, Gerhard Karner, alikutana jijini Vienna na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Tom Berendsen, Waziri wa Hifadhi na Uhamiaji wa Ugiriki, Thanos Plevris, pamoja na Waziri wa Uhamiaji na Utangamano wa Denmark, Morten Boedskov.
Kituo hicho kinakusudiwa kuwapokea waombaji wa hifadhi ambao maombi yao yamekataliwa na ambao hawawezi kurejeshwa katika nchi zao za asili.
Nchi hizo zinataka mazungumzo yakamilike haraka, ili watu wa kwanza waweze kuhamishiwa Rwanda ifikapo mwaka 2027.
Ratiba hiyo ilitangazwa kupitia taarifa iliyotolewa mwanzoni mwa mkutano na waandishi wa habari ulioongozwa na Kansela wa Austria, Christian Stocker, na mwenzake wa Denmark, Waziri Mkuu Mette Frederiksen.
Comments
0