Zaidi ya watu 30 wamepoteza maisha baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kuzama katika pwani ya Senegal, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali. Juhudi za utafutaji na uokoaji bado zinaendelea, huku wanaharakati wakitaka uchunguzi ufanyike kuhusu namna serikali inavyoshughulikia uhamiaji usio rasmi.
Tukio hilo lilitokea karibu na Kebemer, mji ulioko takriban kilomita 180 (maili 112) kaskazini mwa Dakar. Siku ya Jumapili, wizara ya mambo ya ndani ilitangaza kuwa watu 21 walikuwa wamefariki, huku mtu mmoja pekee akiokolewa akiwa hai.
Baadaye, Shirika rasmi la Habari la Senegal (Senegalese Press Agency) liliripoti kuwa idadi ya waliofariki imepanda hadi 34 “baada ya kupatikana kwa miili zaidi.”
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya ndani, boti hiyo ilikuwa imebeba watu waliokuwa wakijaribu kuhama nje ya utaratibu rasmi. Hata hivyo, wizara haikueleza ni watu wangapi hasa waliokuwa ndani ya chombo hicho.
Katika miaka ya hivi karibuni, maelfu ya watu wamefariki wakijaribu kuvuka kutoka Afrika Magharibi kuelekea Visiwa vya Canary vya Hispania. Kundi la kutetea haki za wahamiaji, Walking Borders, linasema watu 635 walipoteza maisha katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu pekee.
Siku ya Jumatatu, Action for Human Rights and Friendship, shirika lisilo la kiserikali la nchini humo, lilitoa wito kwa Bunge la Taifa kuchunguza “usimamizi wa uhamiaji” wa Senegal.
“Haitoshi tena kusikitikia ajali za kuzama kwa boti, kutangaza hatua za udhibiti na kuhesabu idadi ya waliozuiwa,” kundi hilo lilisema.
Comments
0