Mahakama moja nchini Libya imewatia hatiani watu sita kwa kosa la kutengeneza Captagon, dawa ya kulevya inayoathiri akili, kwa ajili ya biashara haramu. Hii ni hatua ya karibuni katika juhudi za kudhibiti kuenea kinyume cha sheria kwa kichocheo hicho cha jamii ya amfetamini.
Mahakama ya Qubbah, mji mdogo ulioko mashariki mwa Libya, ilimhukumu mshtakiwa wa kwanza kifungo cha miaka 25 jela na kumtoza faini ya dinari 22,000 (takriban dola 3,431 za Marekani, kwa kiwango rasmi cha Benki Kuu ya Libya cha dinari 6.4118 kwa dola moja). Taarifa hiyo ilitolewa Alhamisi usiku na ofisi ya mwanasheria mkuu yenye makao yake Tripoli, inayohudumia nchi nzima.
“Washtakiwa waliobaki walitiwa hatiani bila kuwepo mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha maisha, huku kila mmoja akitozwa faini ya dinari 70,000,” ofisi hiyo ilisema kupitia Facebook. Kiasi hicho ni takriban dola 10,917 za Marekani kwa kila mmoja.
Taarifa hiyo haikutaja kiasi cha dawa kilichohusika, lakini iliambatana na picha za vidonge vya duara vyenye rangi hafifu, vingine vikiwa ndani ya mifuko ya plastiki, pamoja na vifaa vya chuma vya kushindilia vidonge na zana za vipimo.
Captagon, inayojulikana pia kama fenethylline, hufahamika kama ‘kokeni ya maskini’ na ni maarufu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) mwezi Januari, taifa hilo la Afrika Kaskazini limegeuka kuwa kituo kikuu cha kikanda cha kupitishia dawa za kulevya za kemikali (synthetic drugs) na mihadarati mingine.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) ilieleza katika ripoti yake ya Januari kuwa magenge ya dawa za kulevya yametumia vibaya hali ya vurugu iliyoikumba nchi hiyo tangu mwaka 2011.
Libya ilitumbukia katika kipindi kirefu cha migogoro ya ndani na mgawanyiko baada ya aliyekuwa kiongozi wake, Muammar Gaddafi, kuangushwa mwaka huo katika uasi ulioungwa mkono na NATO.
Mwezi Oktoba, kikosi cha kijeshi kinachofanya kazi chini ya Jeshi la Taifa la Libya (Libyan National Army) la kamanda Khalifa Haftar kilikamata zaidi ya vidonge milioni 1.3 vya dawa za kulevya baada ya mapigano ya risasi na wasafirishaji haramu katika mji wa Kufra, kusini mashariki mwa nchi. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, wanajeshi watatu walijeruhiwa katika mapigano hayo.
Comments
0