Raia 27 wa Uganda walioandikishwa kupigana upande wa jeshi la Urusi nchini Ukraine wameuawa au wanadhaniwa kuwa wamefariki dunia. Hayo yamebainika katika barua kutoka ubalozi wa Uganda mjini Moscow kwenda wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.
Barua hiyo, iliyoonekana Alhamisi, inataja majina ya Waganda 11 ambao vifo vyao vimethibitishwa, pamoja na wengine 16 ambao miili yao haikuweza kupatikana popote, hata miongoni mwa wafungwa wa vita.
Ubalozi wa Uganda ulieleza kuwa ulipokea taarifa hizo kutoka wizara ya mambo ya nje ya Urusi kupitia “note verbale”, yaani mawasiliano rasmi ya kidiplomasia. Afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Uganda alithibitisha kuwa barua hiyo ni halisi.
Ubalozi wa Urusi mjini Kampala haukujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Taarifa za wanaume wa Kiafrika kurubuniwa kwenda Urusi kwa ahadi za ajira na hatimaye kujikuta kwenye mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine zimekuwa za mara kwa mara, na kuzua hasira katika nchi kama Kenya, Ghana na Afrika Kusini.
Mwaka jana, Ukraine ilisema kuwa zaidi ya raia 1,400 kutoka nchi zipatazo 36 za Kiafrika walikuwa wakipigana pamoja na vikosi vya Urusi katika ardhi yake, baadhi yao wakiwa wameandikishwa kwa njia ya udanganyifu.
Mamlaka za Urusi zimekanusha madai ya kuwaandikisha raia wa Kiafrika kinyume cha sheria ili kupigana nchini Ukraine.
Comments
0