Serikali yenye makao yake mashariki mwa Libya imepiga marufuku raia wa Iran na Afghanistan kuingia nchini humo kupitia bandari zote za nchi kavu, baharini na viwanja vya ndege, kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na serikali hiyo usiku wa Jumatano.
“Raia wa Iran na Afghanistan wamepigwa marufuku kuingia katika ardhi ya Libya kupitia vituo vyote vya kuingilia vya nchi kavu, angani na baharini,” serikali ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook uliothibitishwa.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itakuwa na jukumu la kutekeleza uamuzi huo na kuwarudisha makwao raia wa Iran na Afghanistan wasio na vibali halali vya ukaazi. Serikali haikutoa sababu ya hatua hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanachama wa balozi na ofisi za kibalozi zilizoidhinishwa pamoja na wanafamilia wao hawahusiki na marufuku hiyo. Msamaha huo pia unawahusu watu wanaofanya kazi katika fani za afya na elimu, mradi wawe wamepata vibali vya kazi.
Hatua hii inapanua vizuizi vya kuingia nchini ambavyo utawala huo wa mashariki uliwawekea raia wa nchi nne za Afrika mwezi Juni. Wakati huo, serikali ya Hamad iliwapiga marufuku raia wa Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia, ikitaja “upangaji upya wa uingiaji wa raia wa kigeni nchini Libya.”
Libya imegawanyika kati ya serikali hasimu za mashariki na magharibi tangu mwaka 2014. Serikali ya Osama Hamad yenye makao yake Benghazi inashirikiana na kamanda wa kijeshi Khalifa Haftar, anayedhibiti eneo la mashariki na sehemu kubwa ya kusini mwa Libya.
Kwa upande mwingine, serikali inayotambuliwa kimataifa ya Abdulhamid Dbeibah, aliyeingia madarakani mwaka 2021 kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ina makao yake jijini Tripoli.
Tangu dikteta Muammar Gaddafi alipoangushwa mwaka 2011 katika maasi yaliyoungwa mkono na NATO, Libya imekuwa njia ya kupitia kwa wahamiaji wanaokimbia vita na umaskini wakielekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zilizokusanywa mwezi Juni, Libya ina wahamiaji zaidi ya 900,000.
Comments
0