Papa Leo XIV anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mjini Roma wiki hii ili kuondoa kivimbe kidogo kwenye pafu lake (lung nodule), baada ya madaktari kukigundua wakati wa vipimo vya hivi karibuni vya afya yake.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye umri wa miaka 71 alitangaza mpango wa upasuaji huo Jumapili, wakati wa hotuba yake ya sala ya Malaika wa Bwana (Angelus) katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Alieleza kuwa timu yake ya madaktari ilipendekeza afanyiwe upasuaji, naye ameamua kufuata ushauri wao.
“Wapendwa marafiki, katika baadhi ya vipimo vya hivi karibuni vya afya, madaktari waligundua kivimbe kidogo kilicho sehemu moja kwenye pafu langu. Kiligunduliwa katika hatua ya mwanzo kabisa na kimejikita vizuri sehemu moja,” alisema.
Papa aliongeza kuwa tarehe ya upasuaji huo tayari imepangwa katika siku chache zijazo, na akawashukuru waumini kwa kumuunga mkono.
“Nawashukuru kwa ukaribu wenu wa kiroho na najikabidhi kwa sala zenu,” alisema Papa.
Kwa mujibu wa Vatikani, upasuaji huo utafanyika katika Hospitali ya Agostino Gemelli Polyclinic, na Papa anatarajiwa kupona ndani ya takriban wiki moja.
Matteo Bruni, mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu (Holy See Press Office), aliwaeleza waandishi wa habari kuwa upasuaji umepangwa kufanyika siku za mwanzo za wiki, na kwamba kipindi cha kupona baada ya upasuaji kinakadiriwa kuwa takriban siku saba.
Viongozi wa kisiasa nao wametuma ujumbe wa kumtakia heri. Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alionyesha mshikamano wake na Papa kabla ya upasuaji, huku Rais Sergio Mattarella akimtakia kupona kwa utulivu na kurejea haraka katika afya njema. Rais wa Israel, Isaac Herzog, naye alimtakia kupona kikamilifu na kwa haraka.
Kivimbe cha pafu ni eneo dogo la tishu zisizo za kawaida ndani ya pafu, ambalo mara nyingi hugunduliwa kupitia vipimo vya picha za mwili (imaging tests). Vivimbe vya aina hii si mara zote husababisha dalili, na vingi havihusiani na saratani.
Papa Leo XIV, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Francis Prevost, alichaguliwa kuwa Papa wa 267 kufuatia kifo cha Papa Francis mwaka 2025. Yeye ni Papa wa kwanza kuzaliwa Marekani, na awali aliwahi kuhudumu kama mmisionari nchini Peru.
Katika hotuba yake ya Jumapili, Papa pia alithibitisha mipango ya kuzitembelea Uruguay, Argentina na Peru mwezi Novemba. Maandalizi ya safari hiyo yanatarajiwa kuendelea wakati Papa akijiandaa kwa upasuaji wake.
Comments
0