Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limethibitisha kuwa limekumbwa na shambulio la kimtandao lililosababisha kuibwa kwa taarifa binafsi pamoja na za kibiashara.
Inaeleweka kuwa tukio hilo halikutokana na hitilafu ya mifumo au teknolojia ndani ya chombo hicho kinachosimamia soka duniani. Badala yake, wahalifu walifanikiwa kufikia nyaraka hizo kwa kujifanya wafanyakazi na kuwatumia vibaya.
Katika taarifa yake, Fifa ilisema: “Fifa inathibitisha kuwa imekuwa mwathirika wa shambulio la kihalifu la kimtandao lililosababisha kufikiwa bila idhini kwa kiasi kidogo cha taarifa binafsi na za kibiashara.”
Shirikisho hilo liliongeza: “Fifa inashirikiana kwa karibu na mamlaka husika, zikiwemo vyombo vya sheria.”
Shirikisho hilo pia lilisema: “Fifa inalaani kwa nguvu zote upatikanaji na uchapishaji wa taarifa kinyume cha sheria, hasa data binafsi.
“Vitendo kama hivyo ni ukiukaji mkubwa na usiokubalika wa faragha, na vinaweza kuwa na madhara makubwa kwa watu wanaohusika.”
Kundi linalojiita Handsome Boy Hacking Club limedai mitandaoni kuhusika na shambulio hilo, na wiki iliyopita lilichapisha picha za skrini za mafaili ya Fifa.
Kundi hilo linadai kuwa lilipata data ya ukubwa wa 12GB. Hata hivyo, uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi hicho ni chini ya asilimia 0.1 ya data yote inayohifadhiwa na Fifa, na kwamba shambulio hilo lililenga taasisi yenyewe badala ya watu binafsi.
Hata hivyo, BBC Sport inaelewa kuwa uvujaji huo haukuhusisha nyaraka zozote zinazohusiana na pendekezo lenye utata la Fifa Forward Enterprise, mpango ulioshindwa wa Rais Gianni Infantino wa kuuza sehemu ya haki za Kombe la Dunia.
Wiki hii, Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England (FA), Debbie Hewitt, aliruhusiwa kuyaona mafaili hayo kwa sharti la kusaini makubaliano ya usiri (non-disclosure agreement).
Comments
0