Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Dakar, tukio la kwanza kabisa la michezo ya Olimpiki kufanyika barani Afrika, iko tayari kuanza licha ya kuahirishwa kwa miaka minne. Hayo yalisemwa Alhamisi na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Kirsty Coventry, aliyekiri kuwa safari ya kufikia hatua hii imekuwa ndefu.
Senegal inakuwa nchi ya kwanza ya Kiafrika kuandaa tukio la michezo ya Olimpiki. Michezo hiyo ya vijana inafunguliwa Jumamosi, ikiwashirikisha takriban wanamichezo 2,700 wenye umri wa miaka 14 hadi 17 kutoka kamati 204 za kitaifa za Olimpiki.
Awali michezo hiyo, itakayoendelea hadi Novemba 13, ilipangwa kufanyika mwaka 2022, lakini ililazimika kuahirishwa kutokana na janga la COVID-19.
“Imefika. Tuna furaha sana. Hili limechukua muda mrefu kufikia,” Coventry aliuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Dakar baada ya kukagua viwanja na kijiji cha wanamichezo kabla ya sherehe za ufunguzi za Jumamosi. “Hatua zote kubwa muhimu tumeshazianza.”
Coventry, bingwa wa zamani wa Olimpiki katika mchezo wa kuogelea kutoka Zimbabwe, ndiye Mwafrika wa kwanza kuiongoza taasisi hiyo, baada ya kuchaguliwa mwaka 2025.
“Timu inaweza kutoa uhakikisho wote kwamba kila mtu yuko tayari kuanza. Binafsi najisikia fahari kubwa. Nilikuwa sehemu ya IOC tulipofanya uamuzi (wa kuipa Dakar michezo hii),” alisema Coventry. “Hatimaye kuwa hapa, inahisi kama jambo lililochukua muda mrefu kufika... na kuona kiwango cha tukio la Olimpiki kikionyeshwa.”
Waandaaji wa michezo ya Dakar walisema walilazimika kukabiliana na matatizo ya nishati na mvua dakika za mwisho, lakini wametoa ruhusa ya michezo kuanza, huku zaidi ya wafanyakazi 6,000 wa kujitolea wakisaidia katika maandalizi.
Kwa mujibu wa waandaaji, ulinzi pia utakuwa mkubwa na utawajumuisha maafisa wa polisi kutoka Hispania na Ufaransa wenye uzoefu kutoka Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Humphrey Kayange, mwenyekiti wa tume ya uratibu ya IOC kwa michezo hiyo, alisema athari za Michezo ya Vijana zinaweza kwenda mbali zaidi.
“Kuiona (Dakar) ikikamilika kumekuwa jambo zuri,” alisema Kayange. “Kinachobaki nyuma ni urithi, miundombinu, viwanja na wataalamu. Tunatumaini kwamba mawimbi ya matokeo hayatafifia. Kuna uwezo na fursa kubwa ya hili kuwa mwanzo unaong’aa.”
Afrika haijawahi kuandaa Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto licha ya nchi kadhaa kuomba hapo awali. Alhamisi, Durban ilitangazwa kuwa mgombea wa Afrika Kusini kwa Olimpiki ya mwaka 2036 au 2040.
Comments
0