Seneta Flavio Bolsonaro na Rais Luiz Inacio Lula da Silva walichuana vikali Ijumaa kuhusu gharama ya maisha na kurushiana mashambulizi ya kibinafsi, katika mdahalo wa mwisho wa urais kabla ya duru ya pili ya uchaguzi itakayofanyika Jumapili. Kila mmoja alijaribu kuwavutia wapiga kura ambao bado hawajaamua katika kinyang’anyiro kilichokaribiana sana.
Bolsonaro, ambaye ni mtoto wa rais wa zamani Jair Bolsonaro, alimtangulia Lula katika duru ya kwanza ya uchaguzi mapema mwezi huu. Hata hivyo, kura za maoni za wiki hii zimeonyesha wawili hao wakiwa karibu sawa baada ya pengo kati yao kupungua.
Katika mdahalo huo uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na kurushwa na Globo, kituo cha televisheni kinachotazamwa zaidi nchini Brazil, wagombea hao walirudia ahadi zao za kampeni. Walijikita katika masuala kama gharama ya maisha, ustawi wa jamii na usalama, huku wakishutumiana kwa ufisadi.
Lula, anayewania muhula wa nne baada ya kurejea madarakani mwaka 2022, ametetea nyongeza za kima cha chini cha mshahara zilizozidi kiwango cha mfumuko wa bei chini ya serikali yake, na kusisitiza kuwa utawala wake umewasaidia mamilioni ya Wabrazil kuondokana na njaa.
Rais huyo alisema Bolsonaro mdogo “ni kama wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani ya kujiunga na chuo kikuu. Wanaweza kukariri mambo, lakini hawawezi kujifunza.” Aliongeza pia kuwa “katika mtaa wa kifahari wenye ulinzi anaoishi Bolsonaro, watu hawalali njaa.”
Kwa upande wake, Bolsonaro alijibu kwa kusema bei za chakula kwa Wabrazil zilipanda wakati wa utawala wa Lula. Pia aliukosoa mpango wa mageuzi ya kodi ulioidhinishwa na serikali ya sasa, akitabiri kuwa sheria hizo mpya zitaongeza mzigo wa kodi kwa walaji.
“Lula hata hakumbuki mara ya mwisho alipokwenda kununua mahitaji sokoni kwa sababu sasa anaishi katika kasri la kifahari,” alisema.
Katika vipindi vya mwanzo vya mdahalo, wagombea hao kwa kiasi kikubwa walibaki kwenye mada zilizopangwa mapema, wakipunguza mashambulizi ya kibinafsi yaliyotawala mdahalo pekee uliotangulia kati yao katika kampeni hii.
Hata hivyo, wakati mmoja Bolsonaro alilazimika kumwomba Lula radhi baada ya kusema kuwa rais huyo huwapa Wabrazil kwa mkono mmoja lakini “huchukua kwa vidole tisa.” Lula alipoteza kidole chake kidogo cha mkono wa kushoto katika ajali alipokuwa akifanya kazi ya kuendesha mashine ya kuchonga vyuma (lathe) kiwandani.
“Sitakubali tajiri fulani, mwenye mwenendo wa kisiasa wenye maswali mengi, aniite ‘vidole tisa,’” alisema rais aliye madarakani, akitaka kauli hiyo ifutwe.
“Lula, kama nimekukosea kwa kukuita ‘vidole tisa,’ basi naomba radhi kwa dhati, naomba radhi kwa dhati,” alisema Bolsonaro. Lakini akaongeza: “Je, utawaomba radhi Wabrazil wanaoteseka kwa ukosefu wa usalama ... wenye madeni?”
Mjadala ulipamba moto katika dakika za mwisho, wakati wagombea wote wawili walipopewa nafasi ya kuzungumza bila msimamizi. Lula na Bolsonaro kila mmoja alijaribu kumhusisha mwenzake na kashfa ya udanganyifu inayoihusu benki ya Banco Master.
Lula alimbana Bolsonaro kuhusu madai ya uhusiano wake na mmiliki wa benki hiyo aliyefungwa jela, Daniel Vorcaro, huku Bolsonaro akimhoji Lula kuhusu tuhuma zinazomhusu mtoto wake na udanganyifu katika mfuko wa pensheni.
Mdahalo huo ulikuwa miongoni mwa matukio ya mwisho ya kampeni, kwa kuwa sheria ya uchaguzi ya Brazil inawazuia wagombea kurusha matangazo ya kampeni redioni na kwenye televisheni kuanzia Jumamosi. Hata hivyo, bado wanaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara hadi saa za mwisho za siku hiyo.
Comments
1Интересный дизайн салона автомобиля создает уют. Look into my webpage: <a href="https://365.expresso.blog/question/dizayn-8o/">особенности промышленного дизайна автомобилей</a>