Wakazi wa jimbo la Alberta wamepiga kura kubaki sehemu ya Canada katika kura ya maoni ya kwanza kabisa ya jimbo hilo kuhusu kujitenga, ikiwa ni ushindi muhimu kwa Waziri Mkuu Mark Carney anayejaribu kuunganisha nchi hiyo katikati ya vita vya kibiashara na Marekani.
Shirika la habari la CBC News, kituo cha taifa kinachofadhiliwa na serikali ya Canada, lilitangaza matokeo usiku wa Jumatatu baada ya asilimia 33 ya kura kuhesabiwa. Wakati wa tangazo hilo, asilimia 76 ya kura zilizohesabiwa ziliunga mkono upande wa “kubaki,” dhidi ya asilimia 23 iliyounga mkono jimbo hilo kuendelea na kura rasmi ya kujitenga. Kura ya maoni hiyo haikuwa ya lazima kisheria (nonbinding).
“Wakazi wa Alberta wamefanya uamuzi wazi,” alisema Waziri Mkuu Mark Carney katika taarifa yake. “Walichagua umoja, kujenga pamoja, na kujaliana.” Aliongeza: “Canada ni kubwa kuliko jumla ya sehemu zake.” Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Alberta, Danielle Smith, aliyetangaza kura hiyo ya maoni Mei mwaka huu akisema ilikuwa “wakati wa kupiga kura, kuelewa dhamira ya wakazi wa Alberta kuhusu suala hili, na kuendelea mbele,” alitoa taarifa usiku wa Jumatatu akisema “amefurahishwa sana” na matokeo ya awali yanayoonyesha uungaji mkono mkubwa wa kubaki Canada. Alisema atazungumza na wakazi wa Alberta siku ya Jumanne kujadili matokeo hayo na “jimbo letu linakoelekea kutoka hapa.”
Kikundi kidogo lakini chenye sauti kubwa cha watu wanaotaka kujitenga kimekuwa kikifanya kampeni kwa miezi kadhaa kutaka Alberta iwe huru, kikidai kuwa utajiri wa nishati wa jimbo hilo unachangia kusaidia maeneo maskini zaidi ya Canada, na kwamba Alberta ingekuwa tajiri zaidi bila urasimu wa serikali kuu ya Ottawa kuzuia maendeleo yake. Wiki iliyopita, Carney aliwaambia watu kwenye mkutano mjini Calgary kuwa kuondoka Canada kungekuwa “ni mchezo hatari utakaosababisha miaka mingi ya mgawanyiko mkubwa,” na kuwasihi wakazi wa Alberta “wapige kura kana kwamba Canada inategemea hilo.” Carney, aliyekulia zaidi Alberta, alikiri kuwa wakazi wa Alberta mara nyingi wamekuwa wakijihisi kupuuzwa na serikali kuu ya Ottawa, na akasema serikali yake imeidhinisha mradi mpya wa bomba la mafuta, akiongeza kuwa Alberta ni muhimu katika kusaidia Canada kupunguza utegemezi wake kwa Marekani.
Kura hii ya maoni ya Alberta inafuatia kura mbili za awali za kujitenga katika jimbo la Quebec, linalozungumza Kifaransa zaidi, ambapo wakazi wa Quebec walipiga kura kubaki Canada katika nyakati zote mbili. Makundi ya Wenyeji wa Asili (First Nations) pia yamepinga wazo la Alberta huru, kwani mikataba yao ya ardhi na Ottawa ilikuwepo kabla ya kuundwa kwa jimbo hilo ndani ya Canada. CBC News iliripoti mahudhurio makubwa kutoka kwa Wenyeji wa Asili. Kituo kimoja cha kupigia kura kusini mwa Alberta, katika eneo linaloishi Taifa la Siksika, kiliishiwa na karatasi za kura kwa muda, na kisha kikaendelea kufunguliwa hadi baada ya saa nne usiku kwa muda wa huko ili kuhakikisha kila mtu aliyekuwa foleni anapata nafasi ya kupiga kura.
Hata hivyo, kura ya maoni ya Jumatatu haitarajiwi kumaliza harakati za kujitenga Alberta. Kabla ya kura hiyo, baadhi ya viongozi wa kundi la kujitenga walisema wataendelea kutafuta kura nyingine hata kama wengi wa wakazi wa Alberta wangepiga kura ya kubaki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Oktoba 16 na kampuni ya utafiti Angus Reid, asilimia 62 ya wakazi wa Alberta wanaamini “hakutakuwa na mwisho wa harakati za kujitenga” jimboni humo. Kura ya maoni ya Alberta pia ilijumuisha maswali mengine tisa yasiyo ya lazima kisheria kuhusu masuala kama uhamiaji, upatikanaji wa huduma za jimbo — ikiwemo elimu, huduma za jamii na afya — na mahitaji ya kitambulisho cha mpiga kura. Matokeo ya maswali hayo yalikuwa bado yanaendelea kuingia.
Comments
0