Maelfu ya Watunisia walishiriki Jumamosi katika maandamano makubwa zaidi dhidi ya Rais Kais Saied kwa miaka kadhaa jijini Tunis, wakimshutumu kwa kudhoofisha demokrasia na kushindwa kusimamia uchumi wa nchi, hali inayozidisha changamoto zinazomkabili kiongozi huyo.
Maandamano hayo, yaliyoongozwa na Umoja Mkuu wa Wafanyakazi Tunisia (UGTT) pamoja na makundi ya kiraia, yalifanyika wakati nchi ikikabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi, huduma za umma zinazozidi kudorora, kukatika mara kwa mara kwa maji na umeme, pamoja na uhaba wa dawa na bidhaa muhimu.
Saied alijitwalia madaraka makubwa mwaka 2021 na 2022, akivunja bunge, akiwafukuza majaji kadhaa, na kutawala kwa amri maalum — hatua ambazo wapinzani wake waliziita mapinduzi.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Saied ameongeza mkazo wa ukandamizaji dhidi ya mashirika ya kiraia, waandishi wa habari na wanasiasa wa upinzani. Hata hivyo, Saied amekanusha madai hayo, akisisitiza kuwa yeye si dikteta, na badala yake amewashutumu wapinzani wake kwa kuzusha migogoro ya kiuchumi kwa lengo la kuchochea machafuko ya kijamii.
Katika hali isiyo ya kawaida, vyama vya upinzani kutoka pande mbalimbali za kisiasa viliungana na mawakili, madaktari, waandishi wa habari, vijana wasio na ajira na mashirika ya kiraia katika maandamano yaliyopita katika Barabara ya Habib Bourguiba — eneo lililokuwa kitovu cha maandamano ya mwaka 2011 yaliyochochea harakati za Arab Spring.
Maandamano hayo yanawakilisha changamoto kubwa kwa Saied, baada ya miaka kadhaa ya migawanyiko iliyodhoofisha uwezo wa upinzani kuhamasisha umati mkubwa wa watu.
Akizungumza kwenye maandamano hayo, Slah Eddine Salmi, Katibu Mkuu wa UGTT, alisema: “Ukimya hautakubalika tena... dola haiwezi kujengwa kwa kukusanya madaraka yote mikononi mwa mtu mmoja.” Mamia ya polisi waliwekwa katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu.
Waandamanaji walipiga kelele wakisema: “Hakuna hofu, madaraka ni ya wananchi!” na “Magereza yamejaa, watu wana njaa!” Pia walirudia kauli mbiu maarufu ya maandamano ya mwaka 2011, ambayo wakati huo yalikuwa ya amani: “Wananchi wanataka kuanguka kwa utawala!”
Waandamanaji waliitaka serikali kuwaachia huru wakosoaji wa Saied na kukomesha kile walichokiita mashambulizi dhidi ya haki za vyama vya wafanyakazi. Baadhi yao walibeba mabango yaliyoonyesha hasira kuhusu ukosefu wa ajira na uchafuzi wa mazingira.
Yassine Gharseli, mwandamanaji kutoka mji wa Sfax, uliopo umbali wa kilomita 250 (maili 155) kusini mwa Tunis, alisema: “Imetosha! Nchi inaporomoka. Tunateseka kwa kukatika kwa umeme na maji, na mzozo mmoja baada ya mwingine.”
Aliongeza: “Nilitoka Sfax kusimama kwa ajili ya uhuru wangu na sitokata tamaa, hata kama nitakuwa sauti ya mwisho nchini.”
Comments
0