Baraza la chini la bunge la Italia siku ya Alhamisi lilitoa idhini ya mwisho kwa mageuzi ya mfumo wa uchaguzi yaliyopingwa vikali, yanayoungwa mkono na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, ambayo huenda yakawa na mchango mkubwa katika matokeo ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Meloni anasema sheria hizo mpya zinalenga kuongeza uwezekano wa kuwa na serikali imara. Hata hivyo, upinzani wa mrengo wa kati-kushoto unadai lengo halisi ni kuongeza nafasi yake ya kuendelea kushika madaraka.
Katika kura ya siri, wabunge waliupitisha muswada huo kwa kura 227 dhidi ya 164. Muswada huo unaanzisha mfumo kamili wa uwakilishi wa uwiano (proportional representation – PR), pamoja na nyongeza ya viti inayohakikisha wingi wa wabunge kwa muungano wowote utakaopata zaidi ya asilimia 42 ya kura.
Chini ya sheria za awali, takriban theluthi mbili ya wabunge walichaguliwa kupitia mfumo wa PR, huku waliobaki wakichaguliwa katika majimbo kwa mfumo wa mshindi-kuchukua-wote (first-past-the-post), mfumo ambao wachambuzi walisema huenda uliupendelea upinzani.
Baada ya kura hiyo, Meloni aliandika kwenye mtandao wa X: “Tunaanzisha sheria zilizoundwa kukuza uthabiti na mshikamano wa kibunge wa serikali yoyote. Anayeshinda lazima aweze kutawala.”
Katika mjadala mkali, wabunge wa mrengo wa kati-kushoto waliishutumu serikali kwa kukiuka misingi ya demokrasia kwa kulazimisha sheria mpya za upigaji kura kabla ya uchaguzi, kinyume na matakwa ya upinzani.
“Endeleeni tu kubadilisha sheria ya uchaguzi, tutashinda kwa vyovyote vile chini ya mfumo wowote wa upigaji kura,” alisema kiongozi wa chama cha Democratic Party, Elly Schlein.
Mwezi uliopita, serikali ya mrengo wa kulia ya Meloni ilisherehekea karibu miaka minne madarakani, na kuifanya kuwa serikali iliyodumu muda mrefu zaidi nchini Italia tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Hata hivyo, muungano wake sasa uko nyuma ya upinzani katika kura za maoni, huku kundi jipya la mrengo mkali wa kulia, National Future, likimomonyoa uungwaji mkono wa vyama tawala.
Idhini ya mwisho ya mageuzi hayo ilihitaji kura nne za bunge, na ilihitimisha miezi kadhaa ya mivutano ndani ya muungano iliyoibua maswali kuhusu udhibiti wa Meloni juu ya washirika wake kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao.
Mvutano huo ulijikita katika kipengele cha mageuzi kinachowaruhusu wapiga kura kuchagua wagombea wanaowapendelea kutoka kwenye orodha za vyama, jambo ambalo lingepunguza mamlaka ya viongozi wa vyama kuamua nani anachaguliwa. Hatimaye maridhiano yalifikiwa, ambapo wagombea walio juu ya orodha hupewa kipaumbele moja kwa moja, hivyo viongozi wa vyama wanabaki na mamlaka ya kuamua wengi wa wagombea wanaoingia bungeni.
“Kwa wale waliotarajia kuona mrengo wa kati-kulia ukigawanyika, leo tumejibu kwa vitendo: tuko wamoja, tuna mshikamano, na tumedhamiria kutekeleza ahadi tulizowapa wananchi,” alisema Meloni.
Comments
0