Baraza la Wawakilishi la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo lilimchagua Al-Salhin Abdulnabi kuwa spika siku ya Jumanne, akichukua nafasi ya Aguila Saleh aliyeshikilia wadhifa huo kwa takriban miaka 12, huku kutoridhika miongoni mwa wabunge kuhusu uongozi wake kukiongezeka.
Uchaguzi huo ulifanyika siku moja baada ya wajumbe 98 wa baraza hilo kupitisha utaratibu mpya unaomruhusu spika na manaibu wake kuhudumu kwa kipindi kimoja tu cha miezi 12. Uamuzi huo ulikomesha mfumo uliokuwa ukitumika tangu uongozi wa kwanza wa chombo hicho ulipochaguliwa mwaka 2014.
“Kulikuwa na kutoridhika kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wabunge na uongozi uliopita kutokana na makosa mengi. Tulijaribu kuzungumza na uongozi ili kushughulikia masuala haya, lakini bila mafanikio. Miongoni mwa makosa hayo ni maamuzi yaliyofanywa bila kuwashauri wabunge,” mbunge Jebreel Oheida aliliambia shirika la habari la Reuters.
Baraza hilo pia liliwachagua Tarek al-Ashtar kuwa naibu spika wa kwanza na Mesbah Douma kuwa naibu spika wa pili.
Abdulnabi, ambaye anatoka kabila moja na Saleh, anawakilisha mji wa Tobruk ulioko mashariki mwa nchi na amewahi kuongoza kamati ya urafiki kati ya Libya na Uturuki ya bunge hilo. Ana shahada ya uzamili katika uhandisi wa ujenzi.
Libya, nchi inayozalisha kwa wingi mafuta na gesi, imegawanyika tangu mwaka 2014 kati ya tawala hasimu za mashariki na magharibi, huku Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Government of National Unity) inayotambuliwa kimataifa ikiwa na makao yake katika mji mkuu wa Tripoli ulioko magharibi.
Saleh, ambaye ni mshirika wa kamanda wa kijeshi wa mashariki Khalifa Haftar, kwa muda mrefu amekuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kidiplomasia zinazolenga kumaliza mzozo wa Libya.
Libya ina mabaraza mawili ya kutunga sheria. Baraza la Wawakilishi lilichaguliwa mwaka 2014, ilhali Baraza Kuu la Nchi (High State Council) lilianzishwa chini ya makubaliano ya kisiasa ya mwaka 2015 na wajumbe wake walitokana na bunge lililochaguliwa mwaka 2012.
Baraza la Wawakilishi liko mashariki, wakati Baraza Kuu la Nchi liko Tripoli pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Comments
0