Nicaragua inajiondoa katika Bunge la Amerika ya Kati, hatua inayozidi kuitenga nchi hiyo kimataifa wakati ikiendelea kutuhumiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, wizara ya mambo ya nje ilisema imeamua kuukana mkataba wa mwaka 1987 ulioanzisha bunge hilo la nchi sita “kwa kutumia kikamilifu mamlaka yake ya kujitawala.” Wizara hiyo ilisema uamuzi huo unaanza kutekelezwa mara moja.
Serikali ya Nicaragua haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni zaidi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Jumuiya ya Nchi za Amerika (OAS) kupitisha azimio Ijumaa likiitaka mamlaka ya Nicaragua kuwaachia wafungwa wa kisiasa na kurejesha uhuru wa kiraia. Nicaragua ilijiondoa katika OAS mwaka 2023, ikidai kuwa jumuiya hiyo ya kidiplomasia imegeuka kuwa chombo cha uingiliaji wa Marekani.
Mwaka 2025, Nicaragua pia ilitangaza kujiondoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyoitaka jumuiya ya kimataifa kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Nicaragua.
Nicaragua imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu Aprili 2018, pale maandamano ya kijamii yaliyozimwa na polisi yaliposababisha vifo vya zaidi ya watu 350, majeruhi 2,000, maelfu kukamatwa na wengine kukimbia nchi.
Julai iliyopita, serikali inayoongozwa na Daniel Ortega na mkewe, Rosario Murillo, ilitangaza kuwa nchi hiyo haitafanya tena uchaguzi. Ortega amekuwa madarakani mfululizo tangu mwaka 2007, baada ya kuhudumu muhula mmoja wa awali wa urais katika miaka ya 1980.
Comments
0